Dar es Salaam. Watu 14 wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam nchini Tanzania wakikabiliwa na mashtaka manne ikiwemo la kusambaza taarifa zisizohitajika kwenye mitandao pamoja na utakatishaji fedha.
Washitakiwa waliofikishwa Mahakamani hapo leo Jumatano Julia 24, 2019 ni David Simon (32), Michael Joseph (22), Omary Rajabu (23), Ramadhani Issah(35), Adolph Martine (29), Martine Maiko (26), Ajuaye Gerald (23), .
Wengine ni; Adam Christopher (27), Frank Magazi (29), Mathias Godfrey (22), Joseph Mabruck (26), John Mwambusa (50), Hamza Hassan (23), Amosi Mazwile (22).
Wakili wa Serikali ya Tanzania, Nancy Mushumbusi amedai mbele ya Hakimu Mwandamizi, Hamza Wanjahz kuwa katika tarehe tofauti kati ya mwaka 2017 na Mei 31, 2019 katika maeneo ya Sumbawanga mkoani Ruvuma na maeneo mengine ndani ya Tanzania washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.
Katika shtaka lingine kati ya Januari 2017 na Mei 31, 2019 katika maeneo ya Sumbawanga mkoani Ruvuma na maeneo mengine ya Tanzania washtakiwa hao kwa pamoja kwa kujua na kwa makusudi walisambaza taarifa za uongo kwa njia ya ujumbe mfupi kwa kutumia kompyuta kwa lengo la kudanganya umma wakijua kufanya hivyo ni kosa.
Katika shtaka la tatu, Wakili Mushumbusi amedai kati ya Januari 2017 na Mei 31, mwaka 2019 wakiwa Sumbawanga mkoani Ruvuma na maeneo mengine tofauti ndani ya Tanzania washitakiwa kwa pamoja walipanga kusambaza ujumbe usiohitajika kwenye mitandao kwa njia ya kompyuta huku wakijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.
Pia Soma
- Mahakama yaelezwa Lissu anaendelea na matibabu
- Nyama ya nyati yampeleka jela miaka 20
- Mahakama Kuu Tanzania yafuta hukumu iliyowafunga waandishi wa habari
Wakili Mushumbusi amedai upelelezi wa shauri hilo bado haujakamilika hivyo aliomba mahakama ipange tarehe nyingine kwa ajili ya kutajwa.
Hakimu Wanjah ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 7, mwaka 2019 kwa kutajwa na washitakiwa wamepelekwa rumande kutokana na shtaka la utakatishaji fedha kutokuwa na dhamana.