Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

serikali yaweka mazingira rafiki kwa wawekezaji - Kiruswa

Kiruswa Mazingira rafiki ni pamoja na kubadili kanuni, sera na sheria

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Naibu Waziri wa Madini, Dk Steven Kiruswa amesema serikali imekuwa ikitengeneza mazingira rafiki kwa wawekezaji kwa kuboresha sheria, sera na kununi ili wawekeze bila vipingamizi.

Dk Kiruswa alisema hayo wakati wa utiwaji saini wa mkataba wa maridhiano wa utafiti wa gesi ya helium kati ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) na Kampuni ya Rocket Tanzania Limited, uliofanyika chuoni hapo.

Alisema katika kuboresha sheria, sera na kununi hizo inazingatiwa uchimbaji wa madini utakaofanyika uweze kunufaisha serikali pamoja na jamii katika eneo husika, ikiwa ni pamoja na kufungamanisha sekta ya madini na sekta nyingine za uzalishaji.

Aliipongeza kampuni hiyo kwa kutumia wataalam wa UDSM katika kufanya utafiti na huduma ikiwemo utafiti huo wa gesi ya helium.

“Natoa wito katika utafiti huu wataalam kutoka UDSM, Stamico na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) pamoja na wawekezaji kushikamanishwa kwa pamoja ili kila mmoja aweze kuchota maarifa,” alisema.

Naye Makamu Mkuu wa UDSM, Profesa William Anangisye alisema chuo hicho kinatambua nafasi yake katika maendeleo ya jamii hasa katika uzalishaji wa maarifa yanayosaidia kutatua changamoto mbalimbali kutokana na utambuzi huo,

UDSM imepanua wigo wa utafiti, ufadhili na ubunifu ikiwa ni kuongeza ushirikiano na wadau katika sekta mbalimbali kuwa kufanya utafiti kwa ushirikiano wa karibu na wadau ili kutatua changamoto zao moja kwa moja .

“Aidha chuo kina nia ya kuongeza ubunifu na ugunduzi ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kutatua changamoto za jamii ya kitanzania,” alisema.

Alisema utiwaji saini huo unadhihirisha kwa vitendo aliyoyasema hususan nia ya chuo hicho katika kuhudumia jamii.

Kwa upande wake Kaimu Amidi wa Shule Kuu ya Madini na Jiosayansi, Dk Emmanuel Kazimoto alisema mwaka 2017 Tanzania ilipata taarifa za awali kuhusiana na uwepo wa gesi ya helium kwenye bonde la Ziwa Rukwa huko Songwe.

“Tokea kipindi hicho takribani miaka mitano, UDSM kupitia iliyokuwa Idara ya Jiolojia na Idara ya Jiosayansi kushirikiana na Chuo Kikuu cha Oxford ilijikita kufanya tafiti kuhusu uwepo na asili ya gesi ya helium kwenye Bonde la Rukwa.

“Ambapo chuo tulifanikiwa kutengeneza wataalam wawili waliobobea katika rasilimali hii ya gesi ya Helium ambao wako katik ahatua za mwisho za kumaliza shahada za uzamili,” alisema.

Alisema UDSM kimeweza kupata kifaa maalum cha kuchunguza gesi asili ikiwemo Helium kinachoitwa ‘Min Ruedi’ hivyo kukifanya kuwa na uzoefu mkubwa Afrika katika utafiti wa rasilimali hiyo ya gesi ya Helium.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Rocket Tanzania Ltd, Justyn Wood alisema wamekuwa na ushirikiano kwa muda mrefu na Tanzania hivyo utafiti huo wa gesi ya helium wanaufanya kwa kutumia njia za kijiolojia, kijiokemia na kijiofizikia.

Alisema wataalamu hao pia wanapatikana UDSM katika Idara ya Jiosayansi ya Shule Kuu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live