Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zimetajwa athari za kupanda kwa bei ya mafuta nchini

Mafuta Ed Zimetajwa athari za kupanda kwa bei ya mafuta nchini

Fri, 3 Sep 2021 Chanzo: ippmedia.com

Juzi, Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), ilitangaza bei mpya za ukomo za bidhaa za petroli, dizeli na mafuta ya taa  na baadaye ilizisitisha na kutangaza kuendelea kutumika zilizotangazwa Agosti 4, mwaka huu.

Hatua hiyo ya kupanda kwa bei hizo, imewaibua wasomi na magwiji wa uchumi akiwamo Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Ujasiriamali na Uongozi wa Biashara (IMED), Dk. Donath Olomi.

Akizungumza na Nipashe jana, Dk. Olomi, alisema kwa ujumla mafuta yanapopanda husababisha mfumuko wa bei kwa sababu kila kitu kinategemea nishati.

“Ni kitu ambacho kinatakiwa kijulikane ni nyeti sana na kama tunapandisha tuwe na sababu ya msingi kama kupanda kwenye soko la dunia. Bei ikishapanda inakaa pale kwa hiyo hili ni jambo ambalo linahitaji umakini mkubwa ili lisilete athari sekta nyingine,” alisema.

Mchumi nguli Prof. Samwel Wangwe, alisema mafuta yanaingia kwenye sekta nyingi, hivyo bei zinapopanda husababisha athari kwenye sehemu nyingine.

“Si jambo zuri sana kuruhusu bei kupanda namna hiyo, labda ndiyo maana wamesitisha ili wafikirie vizuri. Kama upandaji unahusisha soko la dunia basi hawawezi kufanya lolote, lakini kama ni kodi siyo kitu kizuri,” alisema.

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam, Prof. Honest Ngowi, alisema mafuta ni chanzo cha uzalishaji mali, hivyo bei ikipanda karibu kila kitu nacho kitapanda.

“Kwa sababu hiyo, lazima kila kinachozalishwa kwa kutumia hicho kilichopanda bei, nacho kitapanda, mzalishaji hatakubali kuingia hasara ataipeleka kwa mtumiaji wa mwisho na kusababisha bidhaa na huduma zinazozalishwa na hicho kitu kupanda, kwenye nauli, mashine kama za kusaga itasababisha gharama za uendeshaji kuongezeka pengine hata viwandani.

“Kwa mwananchi wa kawaida mfano akanunua petroli ambayo bei yake imepanda maana yake imekula kipato chake na kinachobaki kwa matumizi mengine kinakuwa ni kidogo zaidi na ule ubora wa maisha ya watu unaweza kushuka.”

Alisema hilo huwahusu zaidi watu ambao wapo kwenye kipato cha chini ambapo ongezeko dogo la gharama ya maisha humuathiri.

“Kuna watu ikiongezeka bei hawataisikia kabisa lakini idadi ya watu itawahusu sana, ni vizuri ilivyoshuka, bei za mafuta zinatokana na soko la dunia kinachozalishwa huko ambapo hatuwezi kuthibiti sana ila kwenye mambo kidogo,” alisema huku akibainisha kuwa kinachoathiri kingine ni kodi zinazowekwa ambazo zikipungua zinaweza kusababisha kushuka.

EWURA juzi kupitia taarifa yake, ilitangaza bei mpya za mafuta ya petroli ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam ilipanda kwa Sh. 84, dizeli Sh. 29 na mafuta ya taa bei iliongezeka kwa Sh.18.

Chanzo: ippmedia.com