Dar es Salaam. Siku chache baada ya Bonde la Mto Wami/Ruvu kutangaza kusudio la kuzifikisha mahakamani hoteli na kampuni zilizochimba visima bila kibali na kutolipa ada, gharama hizo sasa zimetajwa.
Licha ya hilo wananchi kadhaa jijini hapa, wamekuwa wakishangazwa na jambo hilo huku wengine wakisema ‘tulidhani maji ni mali ya Mungu.”
Gharama ya kusajili ombi la kuchimba kisima jijini Dar es Salaam kwa matumizi ya nyumbani ni Sh60,000 na Sh150,000 kwa matumizi makubwa.
Ofisa wa maji wa bonde hilo, Simon Ngonyani alisema jana kuwa Sheria ya Usimamizi wa Maji ya mwaka 2009 inamtaka kila mtu au taasisi inayochimba kisima kuwa na kibali na kulipa ada ya kila mwaka kulingana na kiasi cha maji kinachovunwa kwenye kisima chake.
Kutokana na hilo, Mwananchi jana lilishuhudia watu mbalimbali wakiwa wamejitokeza katika ofisi za bonde hilo kupata maelekezo ya namna ya kulipia ada hizo.
Pamoja na mwitikio huo baadhi ya wamiliki wa visima wameeleza kuwa hawajapewa elimu na hawafahamu kama wanapaswa kuwa na vibali au kulipia kodi.
Mwananchi lilipita maeneo mbalimbali yenye visima jijini Dar es Salaam na kuzungumza na wamiliki ambao walieleza kwamba hawana wanachokijua kuhusu sheria inayowataka kulipia ada ya maji kila mwaka.
Taarifa ya Bonde hilo inaeleza kuwa ada ya mwaka kwa kisima cha matumizi madogo ni Sh100,000 na matumizi makubwa Sh150,000.
Kwa wafugaji wa samaki, ombi la kuchimba kisima ni Sh60,000 huku ada yake kwa mwaka ikiwa ni Sh100,000 kwa matumizi madogo na Sh250,000 kwa matumizi makubwa.
Mkazi wa Ilala, Mohamed Said alisema amekuwa na kisima nyumbani kwake kwa takribani miaka 25 na hajawahi kusikia kuhusu kibali wala ada.
Alisema atakuwa tayari kufuata utaratibu uliotolewa kama mamlaka husika itamuelimisha na kumfafanulia juu ya ada hiyo.
“Serikali ya mtaa ikituelimisha sidhani kama kuna mtu atakataa kulipa, tunalipia vingapi halafu ugumu uje kwenye maji, tunalipia takataka, umeme, kodi ya ardhi sasa tutashindwaje maji?” alihoji Said.
Hoja kama hiyo ilitolewa pia na Juma Chemise, mkazi wa Buguruni ambaye alisema hadi jana alikuwa hajui ada hizo zinamuhusu nani licha ya kusikia kwenye vyombo vya habari.
Kutokana na maelezo hayo ya baadhi ya wananchi, Mwananchi lilifika ofisi za bonde la Wami Ruvu na kukuta idadi kubwa ya watu waliokuwa wakishughulikia utaratibu wa kupata vibali kwa ajili ya visima vyao.
Miongoni mwa waliofika katika ofisi hizo ni mzee mmoja ambaye hakutaka kutaja jina lake ila alisikika akilalama na kuhoji uhalali wa kulipia maji.
“Mimi najua maji kuyatafuta ukishayapata ni mali ya Mungu sasa leo tunaambiwa tulipie... haya ngoja tusikilize nimekuja kujua utaratibu ukoje,” alisema mzee huyo.
Mhaidiolojia wa bodi wa bonde hilo, Halima Abdalla alisema wameshapokea maombi ya kupata vibali zaidi ya 80 ndani ya siku mbili kuanzia juzi.
Alisema maombi hayo yana jumisha visima vya taasisi, kampuni, hoteli, vituo vya mafuta na watu binafsi.
Alisema licha ya wananchi kuonyesha mwitikio, bodi bado inaendelea kuandaa taratibu za kisheria ili watu wote watakaobainika kukiuka agizo hilo wafikishwe mahakamani.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, Profesa Kitila Mkumbo alikiri kuwa kuna wananchi hawaelewi kuhusu sheria hiyo ya uchimbaji wa visima.
Alisema tayari wizara yake imeshaanza kuandaa utaratibu wa kutoa elimu.