Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zao la kakao lilivyogeuka lulu kwa wananchi Kyela

Zao La KAKAO Zao la kakao lilivyogeuka lulu kwa wananchi Kyela

Thu, 20 Jun 2024 Chanzo: Mwananchi

Wakati wakulima wa kakao mkoani Mbeya wakichekelea bei nzuri ya zao hilo, Chama Kikuu cha Ushirika wilayani Kyela (Kyecu) kimesema hakijafikia kiwango cha uzalishaji kinacholengwa kutokana na mahitaji makubwa ya bidhaa hiyo duniani.

Hii ni baada ya kuwapo kwa bei mpya ya kako inayoonekana kuchochea kilimo hicho ambacho kinatajwa kuwa cha kwanza wilayani Kyela katika kukuza uchumi, kikifuatiwa na mchikichi na mpunga.

Katika mnada uliofanyika Juni 18, 2024 kwa mfumo wa stakabadhi ghalani bei ya kakao ilifikia Sh26,130 kwa kilo kutoka Sh4,860 ya mwaka jana na kufanya wakulima kufurahishwa na bei hiyo na kuhamasika kuendeleza kilimo hicho.

Ponsian Jafeth, mkulima wa zao hilo, amesema licha ya mvua iliyonyesha kuathiri kwa kiasi fulani uzalishaji, lakini bei ya sasa inahamasisha kuongeza nguvu kwenye kilimo hicho.

“Hii bei ambayo kila mkulima hapa Busokelo anafurahishwa nayo, japokuwa fedha haijawahi kuwa nyingi, tumehamasishwa zaidi na kilimo hiki na lazima tuendelee kuangalia namna ya kuboresha zaidi,” amesema Jafeth.

Kwa upande wake, Yusuph Mwamakula amesema pamoja na ongezeko la bei hiyo, wakulima wanaomba Serikali iendelee kutengeneza mazingira ya soko ili mkulima azidi kunufaika na kilimo.

“Tunawekeza nguvu nyingi, hivyo Serikali izidi kutanua wigo katika kutafuta masoko ili wakulima tuendelee kunufaika na shughuli hii, kakao kwa sasa ndicho kilimo chenye kuinua uchumi wetu,” amesema mkulima huyo.

Naye Obedi Mwakatoga 'Kapiki' amesema pamoja na mafanikio ya mwaka huu, wamekutana na changamoto ya kukauka kwa miti na kuoza kwa matunda, jambo lililowapa ugumu kufikia malengo.

Amesema zao la kakao wilayani Kyela halitumii dawa wala kemikali yoyote kwa maelekezo ya wataalamu, badala yake ni kufanya upalizi wa majani ili kuupaya mti kwenye ukavu.

“Kwenye bei, tunaishukuru Serikali, mwaka jana bei elekezi ilikuwa Sh4,200 baadaye ikawa Sh10,000 lakini kwa sasa ni wazi tunaona matunda yake, bei imefikia Sh26,130, tunachekelea,” amesema.

“Tumekuwa na tatizo miti kukauka bila kujua shida, matunda nayo yanaoza haswa kutokana na mvua kubwa iliyonyesha kwa kuwa tunaelekezwa kutolima nyasi badala yake tukate ili kuupa mti nafasi ya kutopata unyevu,” amesema Kapiki.

Hata hivyo, mkulima huyo maarufu wa zao hilo wilayani Kyela, ameongeza kuwa katika kulinda bei hiyo, Serikali inapaswa kutoa elimu kwa wakulima ili kupata uzalishaji bora na tija ili kuliteka soko la ndani na nje.

Wataalamu wafunguka

Ofisa Kilimo wilayani Mbarali, Keneth Nzilano amesema mabadiliko ya sasa katika kilimo hicho yametokana na mkakati wa kitaalamu kwa wakulima kuendesha kilimo kitaalamu ili kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi.

Ameeleza, wanaendelea kuipa nafasi kakao, kama zao la kiuchumi wilayani Kyela pamoja na mazao mengine ya kimkakati, mchikichi na mpung ili kuwanufaisha wananchi hasa wakulima.

“Tunayo mazao matatu ya kimkakati, hasa kakao kama namba moja, mchikichi na mpunga, tutaendelea kuyapa nafasi kwa kuwapa elimu wakulima ya namna ya kulima kwa tija na kuzalisha kwa ubora,” amesema Nzilano.

Ofisa huyo ameongeza kuwa mara kadhaa hutokea changamoto ya hali ya hewa ambapo wananchi na wakulima hushauriwa kulima mazao ya muda mfupi kama viazi, mahindi na mengine yenye kuhimili mvua.

Amesema kakao ina faida nyingi kwani mbali na matumizi ya kinywaji, hutumika pia kutengenezea mafuta na sabuni, japo ni kwa kiasi kidogo na kwamba kadri teknolojia inavyokua matumizi mengine huibuliwa.

“Hivyo, niwasihi wakulima kuchangamkia sana fursa hii ya kakao, watu wasiitumie tu kwa kinywaji, bali hata kutengenezea mafuta na sabuni, tunaamini kadri miaka inavyoenda tutazalisha kwa kiwango kikubwa,” amesema mtaalamu huyo.

Kiwango cha uzalishaji

Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika (Kyecu), Julius Mwakenja amesema pamoja na uzalishaji kupanda kutoka tani 9,000 hadi 12,000, hawajafikia kiwango kinachohitajika cha tani 20,000 hadi 50,000.

Amesema kwa sasa wanaendelea kutoa elimu ya uhamasishaji wa kilimo hicho kwa tija kwa kupanda miti, kwani yapo maeneo yanayostahili kulimwa zao hilo lakini yanapandwa mahindi.

“Uzalishaji na bei vimeongezeka lakini bado hatujafikia kiwango stahiki, soko la dunia linahitaji zao la kakao, hivyo lazima maeneo yote wakulima wachangamkie fursa hii,” amesema na kuongeza.

“Kumekuwa na mabadiliko kwenye matumizi ya miti ya zamani, kwa sasa tunazalisha na kugawa miche ya kisasa kwa wakulima kwa msimu huu zaidi ya miche 15,000 imegawiwa,” amesema meneja huyo.

Hata hivyo, amewataka wakulima kuendelea kuzalisha zao hilo kwa ubora, akieleza kuwa hawataruhusu kuingiza ghalani mzigo usio bora, hivyo wazingatie elimu inayotolewa na watalaamu ili kunufaika na kilimo hicho.

Amesema katika maghala matatu, Kyela ndio kinara hadi sasa kwa kupokea tani nyingi ikilinganishwa na mengine ya Busokelo na Rungwe.

“Katika mnada wa juzi, Kyela ilikuwa na tani 8,954, Busokelo 2,185 na Rungwe tani 795,” amesema Mwakenja.

Chanzo: Mwananchi