Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zao la chikichi linavyomwaga fursa za kiuchumi Kyela

02f472373fdd4783a6ad2b411896022e Zao la chikichi linavyomwaga fursa za kiuchumi Kyela

Tue, 18 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

“TUNAISHUKURU Serikari kupitia TARI (Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania) kwa kutuletea mbegu za michikichi zilizoboreshwa za aina ya ‘tenera’ ambazo zina uwezo mkubwa wa kutoa mafuta mengi tofauti kabisa na ile mbegu ya kienyeji ambayo uzaaji wake hauna faida ya kuridhisha.”

Ndivyo anavyosema mmoja wa wakulima wa michikichi na mkazi wa Kijiji cha Kikusya kilichopo wilayani Kyela katika Mkoa wa Mbeya, Etsoni Mwaipungu, akiishukuru Serikali kupitia Tari kwa kuwahamasisha na kuwasaidia yeye na wakulima wenzake kijijini hapo katika uzalishaji wa chikichi.

Mwaipungu anasema, michikichi iliyopo iliyotokana na mbegu za kienyeji, imechoka kwa kuwa ilipandwa miaka mingi iliyopita hivyo, uwezo wake wa kutoa mavuno, sasa ni mdogo ukilinganisha na miche iliyoboreshwa ambayo wameelekezwa na watafiti kutoka Tari.

Kwa mujibu wa mkulima huyo, kutokana na kukaa muda mrefu, michikichi ya asili haitoi mafuta mengi huchukua muda mrefu tangu kupanda hadi kuanza kuvunwa tofauti na ilivyo kwa michikichi itokanayo na mbegu zilizoboreshwa zinazoanza kuvunwa baada ya miaka mitatu tangu kupandwa shambani.

Anasema baada ya kupata elimu juu ya upandaji na utunzaji wa zao hilo, wakulima wengi wamejitokeza kulima michikichi na sasa kuna uhitaji mkubwa wa mbegu (miche) bora ya zao hilo.

Ikumbukwe kuwa, Mbeya ni miongoni mwa mikoa nchini yenye udongo unaofaa kwa kilimo cha chikichi kwani udongo katika mikoa hiyo ni wenye rutuba ya kutosha na unapitisha maji kwa urahisi.

Ndio maana wakulima wengi kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali mkoani humo, wanaiomba serikali na wadau wengine wakiwamo wataalamu na wazalishaji wa mbegu bora, kuwapelekea mbegu zilizoboreshwa kwa kiwango cha kutosha ili wazitumie kuendesha kilimo kwa tija.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, amekuwa akihamasisha uzalishaji wa zao la chikichi ili kuziba pengo lililopo nchini la mafuta ya kupikia.

Taarifa za vyanzo mbalimbali zinabainisha kuwa, Tanzania huagiza tani 365,000 za mafuta ghafi ya kupikia kwa mwaka.

Toka janga la corona liingie, upatikanaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje umekuwa pia wa kusuasua, hali ambayo imesababisha bei kupandwa mara kwa mara.

Majaliwa anasema: "Hali hii inaweza kukoma endapo Watanzania tutaongeza uzalishaji kwa kutumia kanuni bora za kilimo cha chikichi…”

Mariam Athumani ambaye ni mjasiriamali na mkazi wa Kijiji Kikusya, anasema yeye na wanawake wengine wawili wamelitumia zao la chikichi kama fursa kwani sasa wamejiajiri kukamua mafuta ya kupikia na kutengeneza bidhaa mbalimbali zikiwemo sabuni na mafuta ya kupaka kutokana na zao hilo.

Anasema: “Bado tunatumia michikichi ya asili ambayo haitoi mafuta mengi… Kwenye mikungu kumi ya chikichi, tunaweza kupata dumu mbili za lita 20…”

“Hata hivyo, tumehamasika kupanda miche iliyoboreshwa kutoka Tari ili tuongeze uzalishaji zaidi wa mafuta haya na vitu vingine vinavyotokana na chikichi ili tuongeze kipato chetu na familia zetu…”

Kwa mujibu wa Mariam, kwa sasa mapato wanayoambulia ni kidogo ukilinganisha na uwingi wa mikungu sambamba na nguvu wanayotumia kufanya uzalishaji, hivyo wanaiomba serikali iwapelekee miche bora na mingi zaidi ili waitumie katika kilimo na kuzalishakwa tija.

Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyela, Kenneth Nzilano, anasema uongozi wa halmashauri unaendelea kuunga mkono juhudi za Waziri Mkuu Majaliwa kwa kuhamasisha uzalishaji wenhye tija wa zao la michikichi ili nchi ijitosheleze kwa mafuta na kuwawesha wakulima kupata kipato kikubwa zaidi maana hiyo ni fursa.

Anasema anaishukuru serikali kupitia Tari kwa kuwapelekea wakulima miche bora ya zao hilo.

Kwa mujibu wa Nzilano, uongozi wa halmashauri hiyo unaamini kupitia zao hilo, uzalishaji utaongezeka na kwamba, hiyo ni fursa ya kiuchumi kwa wanachi wa Kyela kwani itasaidia pia kuongeza ajira kwa wananchi wilayani humo na kuiongezea halmashauri mapato.

Anasema Waziri Mkuu Majaliwa ameweka nguvu nyingi katika eneo hilo akilenga kupunguza gharama za uagizwaji wa mafuta ya kupikia kutoka nje ya nchi.

Nzilano anasema wao kama halmashauri, wameamua kuweka nguvu kubwa kuhamasisha wakulima kulima na kutumia mbegu zilizoboreshwa ili waongeze tija katika kilimo chao yaani, wapate zaidi katika eneo lilelile.

“Pamoja na miche ambayo tumeletewa na Tari- Uyole, na sisi tumeendelea kuagiza miche kutoka Tari- Kihinga ili kukidhi mahitaji japo uhitaji wa mbegu bado ni mkubwa,” anasema ofisa kilimo huyo wa halmashauri.

Anawataka wakulima wanaohitaji mbegu za michikichi kufika katika ofisi za kilimo ili kupata ushauri wa kilimo cha zao hilo ikiwa ni pamoja na kupata mbegu (miche) bora.

Hata hivyo Nzilano anasema, mbegu bado zinapatikana katika Tari katika Kituo cha Kihinga na kwamba, wakulima wanatakiwa kufika ofisini ili ofisi ipate idadi ya miche inazopaswa kuagizwa.

Anasema michikichi iliyoboreshwa itawasaidia kuboresha miche mizee iliyopo wilayani humo na kwamba, wanaamini uzalishaji utaongezeka kutokana na mche mmoja ulioboreshwa kuwa na uwezo wa kutoa kati ya lita 25 na 28 za mafuta.

“Licha ya watu wa Tari- Uyole kuleta miche, sisi halmashauri pia mwaka huu tumeagiza na kusambaza miche 4416 kutoka Tari -Kihinga na kutoa elimu kwa wakulima 122,” anasema.

Nzilano anaongeza kuwa, halmashauri imepokea mbegu nyingine 30 kwa ajili ya kuotesha kutoka Tari- Kihinga na kwamba, bado mahitaji zaidi ya miche ni makubwa kwa wakulima wengi wamehamasika kupanda miche iliyoboreshwa.

Naye Bwana Shamba anayesimamia Mazao katika Wilaya ya Kyela, Benard Kibata, anasema shamba liloanzishwa na Tari- Uyole, limeleta hamasa kubwa.

Anasema, hamashauri yao inalitumia kama shamba darasa kuwafundishia wakulima na wengi wamehamasika kulima chikichi baada ya kuona maendeleo ya miche iliyopandwa na taasisi hiyo.

Kwa mujibu wa Kibata, chikichi ni zao linaloleta fursa nyingi za kiuchumi kwa wananchi kijijini hapo kwa kuwa baadhi ya watu hufanya shughuli za ukamuaji mafuta na kuwauzia wenzao kwa Sh 1,200 kwa lita moja na Sh 25,000 kwa lita 20 kwa bei ya mitaani.

“Hata uhaba wa mafuta ya kula uliojitokeza hapa nchini, haukutuathiri sisi kama mkoa…” anasema Kibata.

Anasema mwaka huu wamewasiliana na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) pamoja na Tari-Kihinga ili kuhakikisha miche inapatikana kwa wingi na kwamba, wamekuwa na usimamizi wa karibu kwa wakulima wanaonunua miche hiyo ili waipande ipasavyo.

Mtalaamau huyo anawahimiza wakulima kuchamgamkia fursa hiyo kwa kuhakikisha wanafanya kilimo-biashara.

Anasema: “Mbegu hizi ni bora na zina uwezo mkubwa wa kutoa mafuta mengi, hivyo kuwasaidia wakulima kujikwamua kiuchumi kutokana na ukamuaji wa mafuta pamoja na utangenezaji wa bidhaa mbalimbali kutokana na zao hilo zikiwemo sabuni.”

Mmoja wa watafiti wa zao la michikichi kutoka Tari- Uyole, Beata Paulo, anasema katika zao la chikichi kuna aina tatu ambazo ni ‘dura’ ambayo ni michikichi ya asili.

“Kwa uzalishaji wa mafuta, hii ina uwezo wa kutoa tani moja mpaka moja na nusu kwa hekta moja,” anasema.

Anataja aina ya pili kuwa ni ‘pisifera.’ Hii hutumika katika uchavushaji kati yake na dura, hivyo kupata mbegu bora aina ya ‘tenera’ yenye uwezo wa kutoa tani nne hadi tano kwa hekta moja.

Anasema : “Hii hutumia muda mfupi wa takriban miaka mitatu kupata mazao ya kwanza ukilinganisha na michikichi ya asili...”

Beata anasema lengo la taasisi hiyo ni kuzalisha miche bora ili kukabiliana na changamoto ya uhaba wa miche bora kwa Kanda wa Nyanda za Juu Kusini ili wakulima wapate miche hiyo kwa gharama nafuu kuliko hali ilivyo sasa wanapoagiza kutoka Tari- Kihinga mkoani Kigoma.

Mkurugenzi wa Tari- Uyole, Dk Tulole Bucheyeki, anasema ili uzalishaji wenye tija upatikane, lazima kuwepo watu wa kuzalisha hivyo, kinachotakiwa sasa ni kuboresha miundombinu ikiwemo viwanda vya uzalishaji.

Dk Bucheyeki anasema, wao kama taasisi, wana mpango mkakati wa miaka mitano kuhakikisha upatikanaji wa mbegu bora za mazao mbalimbali unakuwa mkubwa zaidi ukiwemo wa mbegu za michikichi.

Anasema: “Mbegu bora za zao la chikichi zipo za kutosha hivyo, wakulima waje kupata mbegu hizi bora ili wazalishae kwa tija.”

Chanzo: www.habarileo.co.tz