Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng'enda amewataka wakulima wadogo wa chikichi mkoani Kigoma kulipa kipaumbele zao hilo ili kuunga mkono mpango wa serikali wa kulifanya zao hilo kuwa la kimkakati na kuinua uchumi wao.
Alitoa rai hiyo juzi wakati akigawa miche ya michikichi kwa wakulima wanachama wa Chama cha Ushirika wa Mazao (Wami Amcos).
Alisema serikali imeamua zao la chikichi kuwa la kimkakati ili kukabiliana na uhaba wa mafuta nchini, hivyo kuwepo kwa fursa mbalimbali katika uzalishaji wa zao hilo.
Mbunge huyo aliwataka wakulima kuchukua mashamba na miche kwa wingi na kulima zao hilo, kwani mipango ya serikali ni kuweka taratibu mbalimbali za uchakataji na kutoa mafuta yenye viwango vya kimataifa, jambo ambalo litakuwa tija kubwa kwa wakulima wadogo kupata soko la uhakika ndani na nje ya nchi.
Akitoa taarifa kuhusu mpango wa ugawaji miche ya chikichi, Katibu Mtendaji wa Wami Amcos, Kichasa Moka alisema wamepanga kugawa miche 16,350 kwa wanachama wa chama hicho na baadhi kuuza kwa watu binafsi na taasisi ambazo zina uhitaji kwa ajili ya kuongeza mtaji wa kuzalisha miche zaidi.
Alisema mpango wa chama hicho ni kupanda miche 60,000 na kugawa kwa wanachama na mingine kuuza kwa watu ili kukabiliana na uhaba wa miche ya michikichi kwa wakulima.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Kilimo (Tari) Kihinga, Mkoa wa Kigoma, Kuzenza Lushinge alisema wamejipanga kuhakikisha wakulima wadogo na wakubwa wanapata miche kwa wakati na kutimiza lengo la serikali la kuongeza uzalishaji wa zao hilo.
Alitaka halmashauri kuwasimamia kwa karibu wakulima wadogo ili kuhakikisha miche hiyo inastawi na kufikia malengo yaliyokusudiwa, kwani mingi kwa sasa haikui vizuri kutokana na utunzaji duni wa mashamba.