Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zanzibar yatenga Tsh.bilioni 30 kuwezesha vituo vya wajasiriamali

Pesa Fedhaddd Zanzibar yatenga Tsh.bilioni 30 kuwezesha vituo vya wajasiriamali

Sat, 12 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Zanzibar imetenga zaidi ya Sh bilioni 30 kwa ajili ya ujenzi wa vituo vya wajasiriamali kufanya shughuli zao za biashara rasmi na kuepuka na usumbufu pamoja na ujenzi wa masoko matatu yatakayowawezesha wafanyabiashara kufanya shughuli zao kwa ufanisi.

Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja, Idrissa Kitwana ameshuhudia utiaji saini wa ujenzi wa majengo ya wajasiriamali wa mkoa huo, Vuga na Jeshi la Kujenga Uchumi, JKU.

Kitwana alisema Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja umepata jumla ya Sh bilioni tatu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vitakavyotumiwa na wajasiriamali katika kuendesha shughuli zao kwa ufanisi mkubwa. Alisema hatua ya ujenzi wa vituo hivyo unakwenda sambamba na kusajiliwa kwa wajasiriamali 2,720 na kupatiwa vitambulisho vitakavyowawezesha kupata mikopo nafuu.

Mapema Mkuu wa Jeshi la Kujenga Uchumi (JKU) kitengo cha miradi ya ujenzi, Haji Ali wa Ali alisema wamejipanga kuhakikisha wanatekeleza mradi huo na kuukamilisha kwa wakati kwa mujibu wa makubaliano yaliyofikiwa na Ofisi ya Mkuu wa mkoa wa Mjini Magharibi Unguja.

Aidha, aliipongeza serikali kwa kuchukua juhudi za kukiamini kikosi cha ujenzi kilichopo chini ya ujenzi wa jeshi hilo ambapo miradi mingi sasa wamekuwa wakikabidhiwa wao. “Kwa ufupi tunaahidi kwamba tutakamilisha miradi ya ujenzi wa kituo cha wajasiriamali kwa wakati na kuzingatia ubora wa viwango,” alisema.

Aidha, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba, Matar Zahoro Masoud aliutaka uongozi wa JKU kujenga vituo viwili vya wajasiriamali ambavyo vitakidhi vigezo na viwango. Zahoro alisema hayo wakati wa utiaji saini makubaliano ya kuanza kutekeleza mradi wa vituo vya wajasiriamali vitakavyojengwa huko Michakaeni na Kipitacho Pemba.

“Ujenzi wa vituo vya wajasiriamali ni matokeo ya fedha zilizotengwa ambazo ni mkopo kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), ahueni kupambana na ugonjwa wa Uviko-19 zikilengwa katika kuleta unafuu kwa wafanyabiashara wetu kufanya kazi zao za ujasiriamali katika mazingira mazuri,” alisema.

Mkuu wa kikosi cha ujenzi katika Jeshi la Kujenga Uchumi Pemba, Meja Jabir Haji Hamza ameipongeza serikali kwa kuwapatia nafasi ya kuonesha uwezo wao katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya ujenzi inayotekelezwa na serikali.

Hivi karibuni Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Zanzibar alisema wakati umefika baadhi ya miradi mikubwa ya ujenzi kukabidhiwa vikosi vya idara maalumu SMZ ambavyo vinao uwezo wa kutekeleza na kusimamia miradi hiyo kwa ufanisi na viwango.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live