Licha ya huduma ya mafuta ya petroli kuanza kupatikana kisiwani Unguja, bado hofu imeendelea kuibuka kutokana na kiasi kidogo kinachodaiwa kutolewa, hivyo kulazimisha wananchi kupanga foleni kupata huduma hiyo.
Kwa siku tatu kuanzia Aprili 14 hadi Aprili 16 mwaka huu Unguja ilikabiliwa na upungufu wa petroli katika vituo vingi vya mafuta, kusababisha adha kwa wananchi na kukosekana huduma muhimu za usafiri.
Sababu iliyotajwa na Mamlaka ya Huduma za Maji na Nishati Zanzibar (Zura) upungufu huo ulisababishwa na kuchelewa meli iliyofuata nishati hiyo katika Bandari ya Tanga, hata hivyo Aprili 15 meli hiyo ilitia nanga Bandari ya Mtoni Unguja.