Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zanzibar kujenga bandari ya kisasa ya abiria

Bandari Znz Pic Zanzibar kujenga bandari ya kisasa ya abiria

Wed, 10 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Changamoto ya msongamano wa abiria katika bandari ya Malindi Zanzibar, huenda ikapata suluhisho baada ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) kuingia mkataba na kampuni ya Zanzibar Ferry Development (ZF Devco), kwaajili ya ujenzi wa bandari ya kisasa ya Mpigaduri.

Hafla ya kusaini mkataba huo imefanyika leo, Jumanne Januari 9, 2024 Ikulu Zanzibar ikishuhudiwa na Rais wa Zanzibar Dk Hussein Mwinyi ambapo bandari hiyo itajengwa kwa kipindi cha miezi 36.

Imeelezwa kuwa bandari hiyo itajengwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza itagharimu Dola za Marekani 250 milioni (Sh627 bilioni) na itakuwa na uwezo wa kuhudumia abiria 8000 kwa siku na kwa mwaka itahudumia abiria milioni tatu.

Awamu ya pili ya mradi huo utagharimu Dola za Marekani 150 sawa na Sh377.2 milioni.

Akizungumza baada ya kushuhudia utiaji saini huo, Rais Mwinyi amesema hatua hiyo italeta ahueni kwa abiria kupata usafiri wa kisasa na kukuza uchumi wa Zanzibar “Hali sio nzuri kuna msongamano mkubwa hata usalama wake ni mdogo hivyo Serikali ina kila sababu kufanya mabadiliko makubwa na mimi sikutaka tuvunje bandari ya Malindi, nilitaka tutengeneze sehemu nyingine ya kisasa,” amesema.

Amesema hiyo ni fursa kubwa ya kibiashara “Na leo tunaingia kwa pamoja makubaliano kunufaika kibiashara na kiuchumi.”

Amesema katika bandari hiyo kuna mambo matano ambapo itakuwa na boti za abiria, teksi za majini, ndege zinaotua kwenye maji na eneo la kuegesha boti.

“Tuna uhakika baada ya kukamilika mradi huu utabadilisha mandhari ya Zanzibar na kuweka usafiri wa umma wa kisasa, tunawashukuru wawekezaji wetu na Mungu atuwezeshe,” amesema Dk Mwinyi.

Amesema hatua hiyo inaonyesha kwa vitendo utekelezaji wa sera ya Serikali kushirikiana na sekta binafsi na huo utakuwa mfano.

Ametumia fursa hiyo kuwataka watendaji wa Serikali kuhakikisha wanatoa kila aina ya msaada kwa wawekezaji hao ili wasikwame, pia amewataka wawekezaji kuzingatia matakwa ya mkataba na ikiwezekana wamalize mradi huo kabla ya muda.

Mkurugenzi wa Bandari ya Malindi, Akif Ali Khamis amesema kupitia mradi huo wanataka Zanzibar kuwa kitovu cha biashara na kuongeza watalii.

Naye Mwanzilishi wa kampuni hiyo, Matthew VanderBorgh amesema wameamua kuwekeza baada ya kuona mazingira mazuri na sera inayoshawishi.

Amesema katika bandari hiyo itaruhusu kufunga nanga kwa boti nne za kasi kwa wakati mmoja na meli za mizigo mbili na itakuwa chanzo kikuu cha uchumi na Zanzibar.

Naye Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Dk Khalid Salum Mohammed amesema itakapokamilika itafungua uchumi wa nchi na kuondosha changamoto ya usafiri kwa wananchi wa Zanzibar.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live