Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zalisheni vifaranga kwa kuzingatia ubora-Serikali

Zalisheni Vifaranga Kwa Kuzingatia Ubora Serikali Zalisheni vifaranga kwa kuzingatia ubora-Serikali

Wed, 14 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayesimamia Sekta ya Mifugo amewataka wazalishaji wa vifaranga vya kuku hapa nchini kuzalishaji vifaranga hivyo kwa kuzingatia ubora wa kitaifa na kimataifa na mahitaji yaliyopo.

Nzunda ameyasema hayo wakati akifungua kikao cha Wadau wa Tasnia ya Kuku kilichofanyika Jijini Dodoma, kikao ambacho kilijadili hali ya upatikanaji na bei ya vifaranga na vyakula vya kuku pamoja na kushuka kwa soko na bei ya kuku wa nyama hapa nchini.

Wazalishaji wa vifaranga vya kuku wametakiwa kujipanga vizuri ili kuhakikisha wanazalisha vifaranga vya kutosha ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani ya nchi na kuanza kuangalia uwezekano wa kuuza vifaranga wanavyozalisha kwenye masoko ya nje ya nchi.

“Anzeni sasa kuzalisha vifaranga vya kuku kuliangalia na mahitaji ya soko la ndani na nje ya nchi, na ili muweze kulifanya hilo ni lazima mhakikishe vifaranga mnavyozalisha vina kuwa na ubora wa Kitaifa na kimataifa,” alisema

Katika kikao hicho majadiliano ya kina yalifanyika kuhusu wajibu wa wazalishaji wa vifaranga, serikali na wadau kwenye mnyororo wa thamani katika kuzingatia ubora, viwango na katika kuhakikisha kunakuwepo na uzalishaji wenye tija.

Pia kikao hicho kilijadili namna ya kupunguza gharama za uzalishaji wa kuku hasa wa nyama kama msingi mmoja wapo wa kuwawezesha wafugaji wadogo na walaji kumudu gharama. Vilevile wadau wamejadili kuhusu gharama kubwa za utengenezaji wa chakula cha kuku ili kuona ni namna ya kuweza kuzipunguza na hivyo kumsaidia mfugaji kupunguza gharama za ufugaji.

Nzunda alisema kuwa Wizara inaendesha vikao hivyo kwa kuwashirikisha wadau kwa ajili ya kutatua changamoto zinazoikabili tasnia ya kuku na kwa kufanya hivyo Wizara inatekeleza mpango wa mabadiliko wa Sekta ya Mifugo wenye lengo la kutatua changamoto zilizopo kwenye sekta, kuongeza uzalishaji na kuongeza mchango wa sekta ya mifugo kwenye pato la taifa.

Aidha, Nzunda amewasisitiza wazalishaji hao kupitia kampuni zao kuwa na mpango mkakati wa mawasiliano wa kampuni ambao utawasaidia katika kuwasiliana na wadau wao kwa kutoa taarifa sahihi kwa wakati. Vilevile kampuni hizo zimeshauriwa kuwa na mkataba wa huduma kwa mteja katika kuhakikisha huduma zinatolewa kwa wakati.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Huduma za Mifugo, Prof. Hezron Nonga amesema kuwa katika kukabiliana na tatizo la soko wadau wameshauri kuwepo na minada na machinjio ya kuku ambayo itasaidia katika eneo la soko kwa kuwa kuku watauzwa mnadani lakini pia watachinjwa katika machinjio bora, hivyo kutakuwa na usalama wa nyama na kuku wataweza kuhifadhiwa vizuri.

Pia Prof. Nonga amewahamasisha wananchi kutumia nyama ya kuku kwa wingi kwa kuwa ni nyama salama kiafya na kwa kuwa kuku ambao wanafugwa hapa nchini hawana tatizo lolote kutokana na ubora wa chakula wanachotumia. Aidha, amewahakikishia wadau hao kuwa serikali inaendelea kudhibiti uingizwaji wa kuku hapa nchini usiofuata taratibu na kudhibiti magonjwa.

Tariq Machibya ambaye ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Mr. Kuku Farmers amesema kuwa wafugaji wa kuku wanatakiwa kupatiwa elimu juu ya namna kifaranga anavyopatikana na utaratibu wa upataji wa vifaranga. Hii itawasaidia wafugaji kwa kutoa oda kwa wakati na wazalishaji kuzalisha vifaranga kwa wakati na hivyo kuondoa malalamiko yanayotolewa kutokana na kukosekana kwa vifaranga. Hivyo ameshauri njia mbalimbali za utoaji elimu zitumike na wazalishaji wa vifaranga pamoja na serikali ikiwemo ya matumizi ya mitandao ya kijamii.

Pia amewashauri wazalishaji wengine kuanza kulima nafaka ambazo zinatumika katika kutengenezea chakula cha kuku ili kupunguza gharama. Vilevile amewasihi vijana kuona na kutumia fursa ya uwekezaji kupitia tasnia ya kuku, kwa kuwa bidhaa hiyo inatumika kila siku hivyo soko lake ni la uhakika.

Katibu wa Chama cha Wadau wa Kuku, Manase Mrindwa ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa namna ambavyo imekuwa ikishirikiana na wadau hao katika kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili. Aidha, ameiomba wizara kuendelea kuwasaidia wadau hao kupitia vyama vyao ili tasnia ya kuku iweze kuwa imara hapa nchini.

Kikao hicho cha Wadau wa Tasnia ya Kuku ni muendelezo wa vikao ambavyo vimekuwa vikijadili maendeleo ya tasnia hiyo kwa lengo la kutatua changamoto zinazoikabili tasnia hiyo. Katika kikao hicho wadau wameweza kutoka na maazimio zaidi ya 12 ambayo yakitekelezwa yatasaidia kupunguza au kuondoa baadhi ya changamoto zilizopo.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live