Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zaidi ya Sh48 bilioni kukarabati meli tatu

Pesa Fedhaddd Zaidi ya Sh48 bilioni kukarabati meli tatu

Sat, 18 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanza. Serikali imetenga zaidi ya Sh48 bilioni kwaajili ya ukarabati wa meli za MV Liemba itakayofanya safari Ziwa Tanganyika, MT Nyangumi na MT Ukerewe zitakazofanya safari Ziwa Victoria.

Pia Serikali imezindua Meli ya 'MT New Umoja Kazi Iendelee' ambayo ilikuwa ikifanyiwa ukarabati tangu Novemba 2021 hadi Novemba 2023 kwa gharama ya Sh21 bilioni chini ya kampuni ya SM Solution kutoka Korea Kusini.

Meli hiyo iliyotengenezwa kwaajili ya kubeba shehena ya mizigo ya mabehewa 22 sawa na tani 1,200 itakuwa inafanya safari zake nchini, bandari za Uganda na Kenya kuzunguka Ziwa Victoria.

Akizungumza Novemba 17, 2023 wakati wa hafla ya uzinduzi wa meli ya MT Umoja Kazi Iendelee na utiaji saini wa mikataba mitatu ya ukarabati wa meli uliofanyika katika Bandari ya Kusini jijini Mwanza, Naibu Waziri wa Wizara ya Uchukuzi, David Kihenzile ametaka ukarabati huo kuzingatia muda wa mkataba.

"Nitumie fursa hii kuwaomba wananchi jiandaeni kutumia fursa hii ya miradi ambayo inatekelezwa na Serikali na popote pale tunapofanya miradi naomba wananchi wenyeji wapewe kipaumbele cha kupewa ajira na nitoe rai kwa kwa viongozi wa mikoa kusimamia vyema na kuhakikisha mnalinda na mnapinga uhujumu uchumi katika miradi hii," amesema Kihenzile

Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Huduma za Meli (Mscl), Eric Hamissi amesema Serikali imeamua kuwekeza katika ukarabati wa meli hizo kutokana na uimara wake na kuokoa gharama ya kujenga au kutengeneza meli mpya.

"Kuna watu walikuwa wananiuliza kwanini Serikali inafanya ukarabati wa meli hii sasa ni wajibu kwamba mbali na meli hizi kuwa na miaka mingi lakini gharama za kutengeneza meli mpya kama hizi moja ni zaidi ya Sh120 bilioni lakini pia baada ya wataalamu kuchunguza meli zilizopo tulibaini bado vyuma vyake vina ubora mkubwa na havina uchakavu ndio maana Serikali ikaamua kuwekeza," amesema Hamissi

Mkuu wa wilaya ya Nyamagana, Amina Makilagi amesema kukamilika kwa matengenezo ya Meli ya MT New Umoja Kazi Iendelee unaenda kuchochea uchumi wa wananchi wa kanda ya ziwa sambamba na kuongeza pato la taifa.

“Pia utaongeza wigo wa kibiashara, uchumi wa nchi kukua, mapato ya meli kuongezeka hivyo na gawio la Serikali kuongezeka na kuwa kubwa, kuongezeka kwa wataalamu wengi watakaoendelea kutekeleza shughuli mbalimbali ,kuongeza ajira na kuimarisha usafiri,"amesema Makilagi

Isyaka Kayoka, Dereva wa magari ya mizigo ya mikoani na Christina William, mfanyabiashara wa dagaa mbali na kuishukuru Serikali wameomba wananchi kuchangamkia fursa ya uwepo wa meli katika kukuza vipato vyao ikiwa ni pamoja na kujiingiza katika shughuli za biashara.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live