Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zabuni ya Sh1.7 bil yaigawa Posta yaibua mvutano Shirika la Posta

28080 Pic+zabuni TanzaniaWeb

Wed, 21 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mvutano unaoelezwa kuwa “ni wa kimaslahi” ndani ya bodi ya Shirika la Posta (TPC) umekwamisha zabuni ya Sh1.7 bilioni ya ununuzi wa magari matano ya kusafirisha vifurushi.

Ofisi ya Waziri Mkuu ililipa Shirika la Posta kibali cha kununua magari hayo matano aina ya Howo tangu Desemba 7, 2017. Magari hayo yana uwezo wa kubeba tani 30. Hata hivyo, TPC imepeleka kazi hiyo kwa Wakala wa Ununuzi Serikalini (GPSA).

TPC iliyoanzishwa mwaka 1994, inatoa huduma za kiposta ndani na nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na miongoni mwa shughuli zake ni pamoja na usafirishaji wa barua, vifurushi na utarishi.

Wafanyakazi wanainyooshea kidole menejimenti na bodi, wakidai imeingilia mchakato na kusababisha uahirishwe mara nne.

Hata hivyo, viongozi wanasema “maneno maneno” ndiyo yanakwamisha mchakato huo kwa kuwa kulikuwa na mazonge mengi ndipo wakaamua kuiachia GPSA kazi hiyo, kwa mujibu wa mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Posta, Haroun Kondo.

“Tunaamini bei pia itapungua kwa sababu wao ni wataalamu wa shughuli hizi,” alisema Kondo.

Wafanyakazi walioongea na Mwananchi wanasema kila wakati Idara ya Ununuzi (PMU) imekuwa ikipokea maelekezo yasiyofuata utaratibu, hivyo kusababisha mchakato huo kutofika tamati.

“Zabuni hii imeshatangazwa mara nne, lakini kila mara kuna kikwazo kinajitokeza. Kuna wakati tuliipata kampuni iliyoshinda na mkataba ukatolewa, lakini baada ya kushtukia kilichokuwa kinaendelea nyuma ya pazia, ukavunjwa,” alisema mmoja wa wafanyakazi aliyeomba kutotajwa jina.

Alisema hiyo ilitokana na baadhi ya wajumbe wa bodi kugundua kuwa bei imeongezwa kwa zaidi ya Sh500 milioni, hivyo kuitahadharisha PMU kuwa makini na zabuni hiyo.

Baadhi ya wajumbe walitilia shaka bei ya zabuni na kuamua kutafuta ukweli kwenye kampuni iliyoshinda.

Wajumbe hao walipeleka oda nyingine kwa mzabuni inayofanana kila kitu na ile iliyopelekwa na bodi na kukuta bei wanayotakiwa kulipa ni pungufu kwa Sh505 milioni, kwa mujibu wa mtoaji taarifa wetu.

Wajumbe wamegawanyika

Chanzo hicho kinasema baada ya kurudisha ripoti hiyo kwenye kikao cha bodi kilichokuwa kiruhusu kutekelezwa kwa zabuni hiyo, majibizano yaliyotokea kiasi cha kumkasirisha mwenyekiti ambaye alimuagiza Hassan Mwang’ombe, ambaye ni kaimu postamasta Mkuu, kuiahirisha.

“Wajumbe wamegawanyika. Baadhi huwa hawahudhurii vikao. Walimchefua mwenyekiti,” alisema mfanyakazi mwingine kwa masharti ya kutotajwa pia.

Hata hivyo, Kondo amekanusha madai kuwa bodi yake haina msimamo mmoja, lakini wajumbe waliliambia Mwananchi kuwa kuna mpasuko.

“Tunachokifanya ni kulisimamia shirika ili liwe na ufanisi mkubwa. Rais (John Magufuli) aliniteua kwa ajili hiyo,” alisema Kondo.

“Ninapoona chochote hakipo sawa na kitazuia mafanikio ya shirika, lazima nichukue hatua.”

Alisema wakati anateuliwa, Septemba 2016, shirika lilikuwa linapata hasara, lakini hatua zilizochukuliwa mpaka mwishoni mwa mwaka 2016/17, zimewezesha kupatikana faida ya Sh1 bilioni hivyo kutoa gawio la Sh250 milioni serikalini.

Kuhusu ununuzi wa magari, alisema awali, waliidhinisha matumizi ya Sh1.25 bilioni, baadaye wakaongeza hadi Sh1.75 bilioni.

Na kuhusu gharama hizo, Mwang’ombe alisema lawama zinatoka kwa wafanyakazi ambao ni ‘majeruhi’ wa mkakati wa kulirejesha shirika kwenye reli.

“Hili shirika ni muhimu sana na watu walizoea kufanya kazi kwa mazoea. Wamekuwa wazito wasioweza kukimbizana na kasi tunayoitaka, hivyo huwa tunawahamisha. Kwa kufanya hivyo, wanaolalamika ni wengi,” alisema Mwang’ombe.

Mwang’ombe pia alisema uamuzi wa kupeleka zabuni hiyo GPSA ulitokana na TPC kutokuwa na wafanyakazi wa kutosha wenye ujuzi kufanikisha jukumu hilo.



Chanzo: mwananchi.co.tz