Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Zabuni Sekta ya mafuta na gesi yawavutia wengi

4a0f01e94474715403463e9efa136e7f.jpeg Wafunguka macho zabuni kwenye mafuta na gesi

Mon, 11 Jul 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maonesho ya 46 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba yamewafungua macho Watanzania na kampuni za kitanzania zinazotamani kufanya kazi kwenye sekta ya mafuta na gesi. Kauli hiyo imetolewa na Umoja wa Wafanyakazi wa Wachimbaji wa Mafuta na Gesi nchini (OGAWOGA) katika banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), katika maonesho hayo.

Akizungumzia manufaa ya maonesho hayo na faida waliyopata kupitia Pura, Mwenyekiti wa Ogawoga, Frank Mwankefu alisema sekta ya mafuta na gesi nchini imeanza kunufaisha kampuni za kitanzania kutokana na Pura kuziwezesha kupata zabuni na kufanya kazi ndani ya sekta hiyo. “Tunashukuru sana Pura, imekuwa na manufaa kwetu na imetushika mkono. Kuna kazi za mafuta na gesi ambazo kampuni za wazawa tulikuwa hatupati.

Zilikuwa zinafanywa na wageni, lakini Pura imesimama imara na sisi leo tunapata kazi,” alisema Mwankefu. Alisema katika maonesho hayo wananchi wengi wanatembelea banda hilo la Pura ambamo Ogawoga na kampuni nyingine mbili wamepewa nafasi ya kushiriki ili kutoa ushuhuda kwa watanzania jinsi walivyoweza kupata zabuni katika sekta ya mafuta na gesi nchini.

“Tulisota miaka mingi bila kupata nafasi katika sekta ya mafuta na gesi, na hii ni sekta mpya kwa Tanzania,” alisema na kuongeza kwamba maboresho ya sera, sheria na kanuni na kupitia Pura sasa wazawa wanapata fursa. Akitoa mfano alisema wao Ogawoga wamepata zabuni ya kusafisha visiwa vya gesi ya Songosongo, zabuni ambayo awali ingepewa kampuni ya kigeni.

“Watanzania wanaotembelea hapa tunawaeleza na wanavutiwa na wapo waliosoma fani za mafuta na gesi. Wameona mwanga sasa na wengi wameelekezwa na Pura jinsi ya kujisajili katika kanzi data yao ili inapotokea zabuni na kazi waziombe kama sisi tulivyoomba na kukidhi vigezo ikiwa ni pamoja na kuwa na leseni hai na viambatanisho vingine,” alisema Mwankefu.

Kiongozi wa Operesheni wa Kampuni ya Solutions Tag, Tumaini Abdallah ambayo ni mojawapo ya kampuni ya wazawa iliyopata zabuni katika kampuni kubwa za mafuta na gesi nchini, alisema kupata nafasi hiyo kwao ni ushindi na ufunguo wa kazi nyingine nyingi.

“Sisi ni kampuni ya Watanzania asilimia 100 tumepata zabuni katika kampuni kubwa ya mafuta na gesi inayofanya kazi hapa nchini, tulipata fursa hii kupitia Pura ambayo ni mamlaka inayosimamia sekta hii,” alisema Tumaini. Awali akizungumzia katika maoneshi hayo, Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau cha Pura, Charles Nyangi alisema wameshazisaidia kampuni tatu za kitanzania katika mwaka wa fedha ulioisha kupata zabuni mbalimbali.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live