Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

ZSSF yashauriwa kuwekeza miradi yenye tija

ZFSSA.webp ZSSF yashauriwa kuwekeza miradi yenye tija

Mon, 15 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAJUMBE wa Baraza la Wawakilishi wameutaka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), kuwekeza katika miradi yenye tija ili kuepuka hasara na kufanya mfuko huo kupoteza mwelekeo na tishio la kufilisika.

Mwakilishi wa jimbo la Chake Chake, Suleiman Sarhani alisema mfuko wa hifadhi ya jamii ni miongoni mwa mikakati na malengo yake ni kujikita katika uwekezaji wa sekta mbalimbali ikiwamo miradi ya kiuchumi na majengo ya ofisi.

Alisema wasiwasi wake mkubwa ni baadhi ya miradi inayotekelezwa na mfuko huo kutoleta tija na matokeo mazuri kwa maendeleo ya mfuko ikiwamo ujenzi wa kiwanja cha kufurahisha watoto Tibirinzi, Pemba.

“Mheshimiwa Spika, nauomba uongozi wa mfuko wa hifadhi ya jamii kujikita katika uwekezaji wa miradi yenye tija ili kuepuka kuingia hasara na kutishia kufilisika,” alisema.

Mwakilishi wa Jimbo la Shauri Moyo, Hamza Hassan Juma, alipongeza uwekezaji wa mfuko huo ambao umejikita katika miradi ya ujenzi wa majengo ya kibiashara.

“Nimefurahishwa na uwekezaji wa miradi ya majengo ya biashara katika maeneo ya mji wa Unguja ambayo yanaweza kuleta faida kwa maendeleo ya mfuko na kuongeza mapato,” alisema.

Naye Mwakilishi wa jimbo la Paje, Jaku Hashim Ayoub, aliutaka uongozi wa mfuko huo kujenga nyumba zenye gharama nafuu ambazo zitanunuliwa na wafanyakazi.

Alisema nyumba zilizojengwa na mfuko huo Mbweni Unguja ni za gharama kubwa na hakuna mfanyakazi wa kawaida mwenye uwezo wa kununua au kukodi kwa ajili ya kuishi.

“Mheshimiwa wakati umefika sasa mfuko wa hifadhi ya jamii ujenge nyumba nafuu zitakazonunuliwa na wafanyakazi ambao ndiyo wachangiaji wakubwa wa mfuko huo ili nao waweze kunufaika,” alisema.

Kwa mujibu wa maelezo ya Waziri wa Fedha na Mipango, Balozi Mohamed Ramia Abdiwawa, mfuko unaendelea kutekeleza miradi mitatu mikubwa ikiwamo ujenzi wa jengo la biashara eneo la Kisonge, lenye gharama za Sh. bilioni 12.4,pamoja na jengo lingine la biashara jirani na Thabit Kombo lenye gharama ya Sh. bilioni 4.6.

Alisema, mfuko huo unaendelea na ujenzi wa hoteli kubwa Mkoani Pemba kwa gharama za Sh. bilioni 3.6 ambayo itaruhusu watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara kupata malazi ya uhakika.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live