Wakati wafanyabiashara wanaoagiza mizigo nje ya nchi kwa mfumo wa CICS wakidai kodi wanayolipa ni kubwa, Mamlaka ya Mapato Zanzibar (ZRA) imebaini udanganyifu unaofanywa na kampuni zinazosafirisha mizigo hiyo, baadhi zikitumia Namba ya Mlipakodi (TIN) ya ndugu au marafiki.
Mfumo wa CICS (Cargo Import Consolidation System) ni utaratibu wa usafirishaji mizigo wa pamoja kutoka nje ya nchi kwa mizigo ya wafanyashara kukusanywa na kuwekwa kwenye makontena tofauti.
Baada ya kufanya operesheni jana, Kamishna wa ZRA, Yussuph Juma Mwenda alisema utaratibu unaotumiwa na kampuni hizo unawanyonya waagizaji wa mizigo michache na ndiyo maana wengi wanakwepa kutoa risiti kwa kuwa wanakosa cha kufidia gharama zao.
Alisema kuanzia leo maofisa wa ZRA wanaanza kuzichunguza kampuni hizo kabla ya kuweka mfumo mzuri, utakaotoa haki kati ya kampuni na wafanyabiashara wanaoagiza mizigo nje ya nchi.
“ZRA haingilii utaratibu wa biashara za watu lakini lazima utaratibu wowote uendane na matakwa ya sheria. Kwa hiyo tumegundua baadhi ya kampuni zinatumia majina ya ndugu zao kusafirisha mizigo na zingine marafiki, hili linaonyesha kuna shida ya kuficha ukweli,” alisema.
“Pili tumegundua mizigo inapokuja, haiji kwa majina ya walioiagiza kutoka nje badala yake inakuja kwa jina moja na ikifika hawapewi nyaraka yoyote tofauti na ile ya kufika mzigo na wengi wamesajiliwa kwenye Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT), hawapewi risiti zinazoonyesha wamelipia kodi ya kuingiza mizigo Zanzibar.”
Matokeo ya kutopewa risiti au nyaraka za kodi walizolipa, yanawakosesha hao haki ya kudai kwenye ZRA na TRA kodi waliyoingizia mizigo yao, hivyo kuwafanya waone kodi ni kubwa na matokeo yake baadhi huacha kutoa risiti.
Baadhi ya kampuni zilizotembelewa na ZRA ni Yuwi, Binsulum, Awai na Alisalama ambazo zimeeleza zinamiliki meli, hivyo husafirisha makontena moja kwa moja si mizigo hiyo.
“Kuanzia kesho (leo) tunaanza kuwachunguza kuona kama kuna kiasi chochote cha kodi kilichofanyika na jinsi ya kuwasaidia kuwa na utaratibu mzuri. Tunawaomba wananchi wa kawaida ambao hawana uwezo kuleta kontena, wanatakiwa wapewe nyaraka za kodi walizolipa ili wazitumie kudai ritani za mauzo,” alisema.
Mwenda alisema kukosa nyaraka kunawafanya walipe kodi kubwa bila sababu, kwa hiyo watawasaidia, kikubwa watoe ushirikiano kwa mamlaka.
Alisema zipo kampuni nyingi zinazofanya biashara katika mfumo huo, hivyo wametoa wiki mbili zijisalimishe ili wazisaidie kufanya biashara katika mazingira yanayokubaliwa na sheria za kodi.
Kauli za wafanyabiashara
Mfanyabaishara anayetumia mfumo wa CICS, Abdul Abdul alikiri mizigo yote kuingizwa kwa jina lake na kodi analipa kwa jina lake.
Alisema wanaoingiza mizigo wanalipia huduma ya usafirishaji na hupewa nyaraka ya kusafirisha mzigo pekee.
Alikiri kwamba hatoi risiti ya gharama za mzigo kwani kazi yake kubwa ni kuusafirisha lakini iwapo watawekewa mfumo mzuri wapo tayari kuutumia.
Kwa upande wake, Binsulum Ali alisema licha ya kusafirisha mizigo, hawana kampuni ya uwakala hivyo wanatumia jina la mtu mwingine lakini mizigo ya wateja ikifika wanaipeleka kwenye ghala lao na wateja huifuta huko.
Alisema wana takribani miaka mitatu wanafanya biashara hiyo.
“Wateja tunawapa nyaraka za kufikisha mzigo, basi, na tunatumia jina la mtu mwingine kusafirisha mizigo sisi hatuna ofisi za clearing,” amesema.
Meneja wa Alisalama Shipping Line, Mohamed Shekhan Masoud alisema wanamiliki meli kwa hiyo wanachukua kontena moja kwa moja kutoka Mombasa, hivyo hawajihusishi na mfumo huo.
Baadhi ya wafanyabiashara wanaoagiza mizigo nje ya nchi walisema hawapewi nyaraka zozote kwa hiyo imekuwa changamoto kubwa, ndiyo maana inakuwa vigumu katika uendeshai wa biashara.
“Kama kwenye nyaraka za wateja hakuna majina yetu inakuwa ngumu kuja kudai ZRA kwa hiyo hilo linakuwa changamoto kubwa, ukitaka uandikiwe jina lako unaambiwa husafirishiwi mzigo wako, sasa utafanyaje na hauna uwezo wa kusafirisha kontena zima?” alisema Abdurahman Ashur, mfanyabaishara wa mazulia.
Nadhifat Omar Rajab, mfanyabiashara wa vyombo alisema licha ya kuwa Zanzibar wanalipa asilimia 15 lakini bado ipo juu kulingana na mzunguko wa biashara, hivyo ni vyema wakapunguziwa kiasi hicho.