Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Z'bar yatajwa kungara zaidi kiuchumi

3aa5c2a397272d9fdcf6a0b30404c2d8.jpeg Z'bar yatajwa kungara zaidi kiuchumi

Thu, 13 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Zanzibar ikiadhimisha miaka 58 ya Mapinduzi, wachumi wamezungumzia Serikali ya Awamu ya Nane ya Zanzibar chini ya Rais Dk Hussein Mwinyi na kuwa kuna mwelekeo mzuri wa kuimarika kwa uchumi kwa miaka mingi ijayo.

Akizungumza juzi wakati anahutubia wananchi wa Zanzibar, Dk Mwinyi akizungumzia mafanikio katika kutimiza ndoto ya mapinduzi katika sekta mbalimbali aliyataja baadhi ya mafanikio kuwa ni udumishaji wa uendelezwaji wa amani, umoja na mshikamano ambao zimekuwa msingi muhimu uliowawezesha kupiga hatua katika sekta zote za maendeleo.

Alisema mwaka jana kasi ya ukuaji wa uchumi iliimarika ikilinganishwa na mwaka 2020, ambapo athari za Covid-19 zilikuwa kubwa zaidi ambapo katika robo ya kwanza ya mwaka 2021 (Januari – Machi) uchumi wa Zanzibar ulikuwa kwa wastani wa asilimia 2.2 ikilinganishwa na asilimia 1.8 ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2020.

Aliongeza katika robo ya tatu ya mwaka 2021 (Julai – Septemba) uchumi ulikuwa kwa asilimia 8.8 ikilinganishwa na asilimia 3.3 kwa kipindi kama hicho katika mwaka 2020 na kusema ongezeko hilo limechangiwa na kuongezeka kwa miradi ya uwekezaji, kuimarika sekta ya utalii pamoja na shughuli za biashara.

“Kwa kipindi cha Januari hadi Novemba 2021, serikali ilikusanya shilingi bilioni 745.1, sawa na ongezeko la asilimia 22 ikilinganishwa na makusanyo ya shilingi bilioni 610.5 zilizokusanywa kwa kipindi kama hicho mwaka 2020 ambapo ongezeko hilo limechangiwa na kuimarika kwa uchumi pamoja na kuanza kutumika kwa mifumo ya kielektroniki ya ukusanyaji wa mapato iliyoanzishwa,” alisema.

Mchumi Profesa Joseph Semboja akizungumza na HabariLEO amebainisha kuwa uamuzi wa kuweka nguvu kubwa kwenye uchumi wa bluu ni uamuzi ambao una tija kubwa kwa mustakabali wa uchumi kwa kuwa kupitia bahari kuna fursa nyingi za kiuchumi.

“Uchumi wa bluu ni eneo ambalo linaweza kutumika vema kuivusha Zanzibar kiuchumi hasa kutokana na fursa nyingi zinazopatikana kwenye bahari na kwa uamuzi wa Zanzibar kuweka nguvu kubwa kwenye eneo hilo kuna faida nyingi ambazo zitaongeza ajira kwa wananchi,” alisema Profesa Semboja.

Alisema kwa uamuzi wa Serikali ya Zanzibar kujenga bandari kubwa na ya kisasa kutawezesha meli kubwa za mizigo kuingia kisiwani humo na kuchagiza maendeleo ya biashara, hatua itakayoimarisha uchumi wa nchi.

Pia alibainisha kuwa kwa kuwekeza kwenye uvuvi ikiwa ni njia mojawapo ya kutumia vema fursa za uchumi wa bluu kutafungua ajira za moja kwa moja na zisizokuwa za moja kwa moja kwa vijana kisiwani humo. Alisema: “Kwa uamuzi wa serikali kuagiza dhana za kisasa za uvuvi zitakazowawezesha wavuvi kwenda kuvua katika maji marefu hakika kutaongeza upatikanaji wa samaki wa kutosha na kuongeza na kuimarisha biashara ya samaki.”

Kwa upande wake Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Nelson Mandela, Profesa Hulda Swai amebainisha kuwa Zanzibar kwa miaka miwili ijayo itazidi kuimarika kiuchumi hasa kama ikiendelea na namna yake ya kujiimarisha kiuchumi. Alisema kutokana na kufahamika kwake kimataifa, zipo fursa nyingi zaidi ambazo zinaweza kufunguka na kusaidia kukua kwa uchumi wa nchi hasa katika nyanja za utalii.

Alisema kwa Zanzibar inaweza kufungua fursa zaidi katika nyanja za utalii hasa kwa kujikita kwenye utalii wa mikutano ambao kwa Zanzibar utaiingizia fedha nyingi kutokana na kujulikana kwake na kuvutia watu wengi kupenda kwenda. “Zanzibar itazidi kuimarika kiuchumi kutokana na mikakati yake ya kutumia fursa za utalii, kuwatumia Wazanzibari waishio nje ya nchi (diaspora) na hata ilivyojikita katika kutumia vema fursa za uchumi wa bluu hakika hiyo ni kati ya mikakati sahihi ya kuinua uchumi wake,” alisema Profesa Hulda.

Naye Ali Yusuph Hamza ambaye ni Mzanzibari anayeishi Temeke- Dar es Salaam amebainisha kuwa udumishwaji wa amani kisiwani humo, kuondoa tofauti za kiitikadi za kisiasa kunasaidia kuimarisha maisha ya watu na kukuza uchumi.

“Kwa sasa Zanzibar imepata kiongozi mwenye uchu wa maendeleo ya nchi yake na ameonesha njia kivitendo na hii inaonekana kutokana na sera zake za kuiinua nchi kiuchumi, sasa ni muda wa kuhakikisha tunatekeleza sera ya uchumi wa bluu na kuimarisha utalii, Wazanzibari tufanye kazi,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live