Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imewatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa mafuta nchini, ikisema yapo ya kutosha siku 55, huku ikieleza sababu za maeneo ya pembezoni kutopata kwa ufanisi nishati hiyo. Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na wanahabari kuhusu upatikanaji wa petroli na dizeli. Hivi karibuni kulitokea changamoto katika miji ya pembezoni kuhusu upatikanaji wa mafuta, jambo lililoibua sintofahamu kwa watumiaji wa nishati hiyo.
Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura), imewatoa hofu Watanzania kuhusu upatikanaji wa mafuta nchini, ikisema yapo ya kutosha siku 55, huku ikieleza sababu za maeneo ya pembezoni kutopata kwa ufanisi nishati hiyo. Mkurugenzi Mkuu wa Ewura, Dk James Andilile alisema hayo jijini Dar es Salaam jana, alipozungumza na wanahabari kuhusu upatikanaji wa petroli na dizeli. Hivi karibuni kulitokea changamoto katika miji ya pembezoni kuhusu upatikanaji wa mafuta, jambo lililoibua sintofahamu kwa watumiaji wa nishati hiyo. Kutokana na changamoto hiyo, mwanzoni mwa wiki hii, Ewura ilizionya kampuni zinazohodhi mafuta ili baadaye kuuza kwa bei kubwa ikisema ni kinyume cha sheria na kanuni zinazosimamia biashara ya mafuta hayo nchini na masharti ya leseni zao za biashara. Hata hivyo, jana Dk Andilile alisema mafuta yapo ya kutosha akibainisha kuwa kuanzia Julai 14 kuna lita milioni 169 za petroli zitakazotosheleza kwa zaidi ya siku 25. Pia, alisema kuna lita zaidi ya milioni 300 yatakayotumika siku 30. “Jana (juzi), tulipita katika baadhi ya maghala ili kujua changamoto ipo wapi kwa sababu mafuta yapo ya kutosha lakini katika miji na pembezoni hayaonekani. Tumeridhia kwamba hakuna changamoto ya mafuta yapo ya kutosha. “Lakini tumegundua vitu vichache kulikuwa na changamoto kwenye maghala kwa magari kuingia na kutoka. Kuna baadhi ya magari yakienda ghala moja wanaambiwa na wapakiaji waende jingine,” alisema Dk Andilile. Pia, alisema muda ambao gari linatoka ghala moja kwenda jingine unasababisha mafuta kushindwa kupelekwa kwa wakati katika maeneo mbalimbali, yakiwamo pembezoni mwa miji. Akifafanua zaidi, Dk Andilile alisema kulikuwa na watu kuhodhi mafuta, huku akitolea mfano kuwa mtu (dereva) anaweza akaambiwa aende ghala A kuchukua, kumbe anatakiwa kwenda B. “Tumepita kwenye maghala tukawaleza kuwa tunajua mchezo wanaoucheza. Tumewaambia hatukubaliani na mchezo wao,” alisema. Hata hivyo, Dk Andilile alisema wamekubaliana na wauzaji wa mafuta, wamiliki wa maghala na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kufanya kazi kwa saa 24 ili kuongeza kasi ya upelekaji wa mafuta kwenye maeneo yaliyobainika na changamoto. “Niwahakikishie mafuta yapo, wafanyabiashara wapo tayari kupeleka nishati hii kwenye maeneo yenye shida. Lakini niseme wale wanaohodhi mafuta kwa matarajio bei itapanda waache mchezo huo, atakayebainika atachukua hatua,” alisema. Mbali na hilo, aliwataka wananchi kuachana na tabia ya kubeba nishati hiyo kwenye vidumu, akisema ni hatari. Pia, alisema ni kosa kwenye vituo kuwauzia watu nishati katika vibebeo visivyoruhusiwa kwa mujibu wa sheria. “Niwaonye wenye vituo vya mafuta wanaopenda kuuza nishati hii kwa utaratibu wa vidumu kuacha mara moja mtindo huu kwa sababu ni hatari. Yule anayeuza na anayenunua wakikamatwa watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Dk Andilile. Alisema meli zinaendelea kushusha mafuta kama kawaida, hakuna changamoto katika mfumo wa kuagiza nishati hiyo. Pia, alisema Serikali imejipanga vema kuhakikisha mafuta yakifika meli zinawekewa utaratibu maalumu wa kushusha kwa ufanisi. Kuhusu upatikanaji wa mafuta kwa Agosti, Kamishna wa Mafuta na Gesi Asilia, Michael Mjinja alisema zabuni zinafanyika kila mwezi na meli zinapangwa kwa utaratibu wa maalumu kwa kushusha, akiwatoa hofu wananchi.