Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Yara kuongeza tija uvuvi, mifugo

Malisho Mifugo Ngombe Yara kuongeza tija uvuvi, mifugo

Thu, 21 Sep 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kampuni ya Yara Tanzania imezindua bidhaa za lishe ya mifugo zitakazochochea ongezeko la kipato kwa wafugaji na wavuvi nchini.

Bidhaa hizo pia zinatajwa zitachochea usalama wa mazingira, kuokoa fedha za kigeni katika uagizaji wa maziwa nje, usalama wa afya na kuongeza mchango wa sekta hiyo katika Pato la Taifa.

Uzinduzi huo ulifanyika jana mkoani Iringa, ikiwa ni siku chache baada ya Tanzania kuwa mwenyeji wa Jukwaa la mfumo wa chakula la Afrika (AGRF), uliochechemua huduma ya chakula kwa uhakika, ubora na utoshelevu.

Bidhaa hizo zinazowezesha unenepeshaji, ukuaji wenye afya, kinga ya magonjwa na virutubisho kwa vipimo tofauti ni pamoja na maziwa Pro, Kynofos 21, Phospro 17, Phossure 12 na Kimtrafos 12 Grande.

Katika wasilisho lake jana, mtaalamu wa lishe ya mifugo kutoka kampuni hiyo, Dk Peter Mukua alisema bidhaa ya ‘Maziwa Pro’ itasaidia ongezeko la lita tatu zaidi kwa ng'ombe kwa siku ikilinganishwa na wastani wa nusu lita hadi lita mbili za maziwa kwa sasa baada ya kuongeza kinga ya mifugo na uboreshaji wa uzazi.

“Maziwa Pro inashughulikia upungufu wa fosforasi unaochangia uzalishaji duni, ina Phosphorous iliyoongezewa nguvu kwa kuchanganywa na molasi (molasses) ya unga na asilimia 15 ya protini,” alisema Dk Mukua.

Kwa mujibu wa Bodi ya Maziwa ya Tanzania (TDB), Tanzania ina upungufu wa uzalishaji wa maziwa wa takriban lita bilioni tisa kwa mwaka ili kukidhi mahitaji ya lita bilioni 12 na mwaka jana Taifa lilitumia Sh23 bilioni kuagiza maziwa ili kukidhi upungufu huo, hali iliyosababisha kupoteza ajira na mapato ya kigeni.

“Kwa bidhaa nyingine kama Kynofos 21 zinatatua matatizo ya maganda dhaifu ya mayai, miguu dhaifu ya kuku, hali inayofanya washindwe kutembea, tatizo la kudonoana wao kwa wao, hususan kwa kuku wa mayai, kasi ndogo ya ukuaji, na ongezeko dogo la uzito kwa kuku wa nyama na nguruwe,” alisema Dk Mukua.

Mkurugenzi Mtendaji wa Yara Tanzania, Winstone Odhiambo alisema kampuni hiyo itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Serikali, wafugaji na wazalishaji wa chakula cha mifugo ili kuboresha wingi na ubora wa uzalishaji wa maziwa, nyama, mayai na samaki.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mifugo, kati ya 2006/07 na 2020/21, ng’ombe waliongezeka kutoka milioni 18.5 hadi milioni 33.9, mbuzi milioni 13.1 hadi milioni 24.5, kondoo milioni 3.5 hadi milioni 8.5 na kuku milioni 30 hadi milioni 87.7, lakini Serikali imekuwa ikikiri tija yake kuwa ndogo.

Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga, alisema sekta ya mifugo imekuwa na mchango wa asilimia saba katika pato la Taifa, kiwango ambacho ni kidogo kulingana na utajiri wa mifugo nchini.

“Sekta ya umma na binafsi zinahitajika kukuza uzalishaji na kuokoa fedha nyingi za kigeni zinazotumika kila mwaka kuagiza maziwa, nyama na mayai,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live