Serikali imeombwa kuridhia mkataba wa kimataifa wa kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani namba 189/2011 na kuweka sheria maalum itakayosimamia ajira ya kazi za nyumbani.
Akizungumza Juni 16, 2023 kwenye maadhimisho ya siku ya mfanyakazi wa nyumbani kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la kutetea haki za wafanyakazi hao la WoteSawa, Angela Benedicto, Meneja wa Nyumba Salama wa shirika hilo, Jaqueline Ngalo amesema uwepo wa sheria utapunguza au kuondoa ukatili kwa wafanyakaza hao. Ametolea mfano wa Januari hadi Juni 2023, wafanyakazi wa nyumbani 165 walifanyiwa ukatili na kuokolewa, kupewa huduma ya malazi, chakula, msada wa kisaikolojia, matibabu na msaada wa kisheria huku 86 kati yao wakirejeshwa kwenye familia zao.
“Kuridhiwa kwa mkataba huo kutasaidia kuimarisha ulinzi, mazingira ya staha yenye usawa wanapofanya shuguli zao na kuwezesha usimamizi mzuri wa kisheria kwa masuala yanayohusu wafanyakazi wa nyumbani,”amesema Ngalo amesema nchini hakuna sheria maalum inayokidhi mahitaji ya wafanyakazi wa nyumbani kwa kuzingatia upeke wa sekta hiyo akidai mfumo wa kisheria wa ajira ni jumuishi kwa wafanyakazi wengi wakiwemo wafanyakazi hao. “Tunaiomba pia Serikali kupitia mamlaka zake husika itekeleze kikamilifu sheria ya ajira na mahusiano kazini ya 2004, sambamba na mkataba wa Shirika la Kazi la Kimataifa (ILO) namba 138/1973 unaoweka katazo la ajira kwa watoto chini ya miaka 14,”amesema Amesema wafanyakazi wa nyumbani wanakabiliwa na mazingira mabaya ya kazi ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwa saa nyingi, kulipwa ujira pungufu au kutolipwa kabisa, kufanya kazi bila mikataba ya kimaandishi, kutopata ulinzi wa kijamii, kutendewa ukatili na unyanyasaji. Ngalo ameishukuru Serikali kuongeza kima cha chini cha mshahara wa mfanyakazi wa nyumbani ambapo Sh250,000 malipo ya mfanyakazi wa nyumbani anayefanya kazi kwa wanadiplomasia au wafanyabiashara wakubwa, Sh200,000 kwa wanaofanya kazi kwa Maofisa wenye stahiki, Sh120,000 kwa wasioishi kwenye kaya za waajiri wao na Sh60,000 wanaoishi kwenye kaya za waajiri wao. Ofisa wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Fortunata Scanda amewataka wafanyakazi hao kutokimbilia kulipiza kisasi pale wanapofanyiwa ukatili badala yake watoe taarifa Serikali za Mitaa, Dawati la jinsia au WoteSawa ili kupata msaada. Naye Ofisa Kazi Mfawidhi Idara ya Kazi Mkoa wa Mwanza, Betty Mtega alilitaka shirika hilo kuwajumuisha wafanyakazi wa nyumbani kwenye sherehe za Siku ya Wafanyakazi Duniani (Mei Mosi) akidai nao wanahaki ya kuisheherekea. Aliwataka waajiri kusaini mkataba wa ajira kati yao na wafanyakazi wao kwakua utasaidia pande zote mbili endapo shida ikitokea mbeleni. Mfanyakazi wa Nyumbani, Neema Ishengoma alilishukuru shirika hilo kuandaa maadhimisho hayo huku akiwataka waajiri kuishi nao vizuri ikiwa ni pamoja na kuwajali, kuwapenda na kuwathamini kama wanavyofanya kwa watoto wao wanaowaachia wakienda kazini.
Katika maadhimisho hayo, yenye kauli mbiu ya ‘Hakuna usawa wa kijamii bila kuwa na kazi za staha kwa wafanyakazi wa nyumbani’, Wotesawa ilitambua mchango wa waandishi wa habari na vyombo vyao kwa kuwatunuku vyeti akiwemo mwandishi wa Mwananchi, Saada Amir.