Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizi mpya Kariakoo tishio

Kariakoo Pic 780x470 Wizi mpya Kariakoo tishio

Wed, 31 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Umewahi kuibiwa na mtu aliyekuja kwako kwa lengo la kukupa msaada? Huo ndio wizi unaoendelea mitaa inayozunguka Soko la Kariakoo jijini Dar es Salaam.

"Huwezi kuingia Kariakoo na gari, ni shida sana, hii nafikiri ndiyo imechangia kuwapa mbinu hii ya kuiba kutoa kwa watu wachache wasiokuwa waaminifu," amesema Mathayo Julius mfanyabiashara wa vyombo eneo hilo.

Amesema wengi wanapokwenda kununua vitu kama vingi, huwa hawawezi kubeba, lazima watafute msaada na hapo ndipo wengi wao wanaibiwa.

Kauli ya mfanyabiashara huyo inakolezwa na tukio la Alhamisi iliyopita, 'binti' mmoja alipoangua kilio Mtaa wa Congo kama amepata taarifa ya msiba.

Binti huyo aliyejitambulisha kwa jina la Neema Jackson amedai kuibiwa mzigo wake wa Sh1.5milioni aliompa mtu aliyejifanya anamsaidia kubeba hadi kituoni kwa ujira wa Sh2,000.

Akielezea tukio hilo, Neema amesema, baada ya kumaliza ununuzi, akiwa njiani kwenda kituo cha daladala, ndipo alitokea kijana na kumsalimia na kuomba amsaidie kubeba mzigo huo hadi anapokwenda.

"Nilikuwa nakwenda kupanda daladala za Ubungo zinazotokea Mnazi Mmoja, akasema nimpe Sh2,000.

"Sijui hata alinipotea vipi, sijui nimeibiwaje," amesema Neema kwa uchungu huku akibubujikwa na machozi.

Neema ni miongoni mwa watu wengi wanaoibiwa eneo hilo kwa staili hiyo.

Naomi Peter anaeleza alivyopoteza mzigo wake wa Sh800,000 kwa staili hiyo.

"Nilipaki gari maeneo ya Big Bon, sababu haikuwa rahisi kuingia nalo hadi kule madukani kutokana na ilivyo ngumu kuingia na gari Kariakoo.

"Nilipomaliza ununuzi, nilihisi nitamudu kuubeba mzigo wangu hadi kwenye eneo nilipopaki gari, lakini mita kama 20 mbele nilichoka, ndipo akatokea kijana na kusema nimpe Sh1,000 ya kula, yeye anisaidie kubeba.”

Ameema, aliona ni jambo zuri, akakubali.

"Tulipofika kwenye Kituo cha Msimbazi, pale kuna zebra, sijui nilijichanganya vipi katika kuangalia kulia na kushoto ili tuvuke, yule kijana sikumuona.

"Nililia siku nzima, lakini sikuwa na cha kufanya, hata nikienda polisi namshtaki nani? Niliishia kulia, siku yangu yote iliharibika nikakubali hasara," amesema.

Wafanyabiashara wa eneo hilo wamesema, watu wengi sana wanaibiwa kwa aina hiyo ya wizi.

"Wanaoibiwa wengi huwa ni watu wa kutoka mikoani, japo hata wa Dar es Salaam wengine wanaibiwa,” amesema Jeremiah Mathias, mfanyabiashara wa khanga na vitenge.

Akisimulia wanavyoibia watu, amesema wako kama mtandao, wanakuwa wawili au watatu na kuendelea.

"Pale, anapokubebea mzigo wako huwa anakusoma, lakini wakati huohuo unaweza kuta kuna mwenzake mbele wanawasiliana, mkifika sehemu yenye msongamano hapo ndipo ukizubaa au kujichanganya tu unaibiwa.

"Wapo wengine wanavaa shati mbili mbili, akishajichanganya kwa watu anatoa ile ya juu, wakati huo mzigo wako kaishampasia mwenzake aliyekuwa akiwasiliana naye, unakuwa huwezi kumkumbuka na kibaya zaidi huwa hakuna ushahidi wakati mnakabidhiana mzigo," amesema Mathias.

Nini kifanyike

Mfanyabiashara mwingine, Nashon Naftari amesema ni vizuri mtu kubeba mzigo wake bila kumpa mtu amsaidie.

"Hii ndio njia rafiki zaidi, kama unajua unakuja kununua mzigo mkubwa ambao utaweza kuubeba mwenyewe njoo na mtu wa kukusaidia ambaye unamfahamu,” amesema Naftari.

"Pia, unaweza kukodi kirikuu au toyo kama mfuko wako unaruhusu, la sivyo vyote umeshindwa basi omba mtu wa kukusaidia hapo kwenye duka ulilofanya ununuzi.

"Mwenye duka atakupa mtu wa dukani anayefahamika, lakini ukitoka tu na kuchukua mtu njiani akusaidie, wengine sio waaminifu ndipo unakutana na hilo la kuibiwa.

"Wengi sana hapa Kariakoo wanalizwa (wanaibiwa) kwa mtindo huo," amesema Naftari.

Hata hivyo, mtindo huo wa watu kujitolea kuwabebea mizigo wanunuzi kwenye masoko umeenea kwenye masoko mengi ya jijini Dar es Salaam kwa ujira wa kuanzia Sh500 na kuendelea.

Mbali na wengi wao kuibiwa, baadhi ya watu wamesema, msaada huo ugeuka mzigo kwao kutokana na heka heka wanazopitia kwa watu waliowapa mizigo yao.

"Ukimpa mzigo wako, kwanza unakuwa kama mtumwa wake, maana huo mwendo anaotembea muda wote inabidi uwe unakimbia ili kwenda naye sambamba," amesema Amina Kassim.

Janeroza Majura amesema aliwahi kufanya hivyo kwenye soko la ndizi Mabibo, alijuta.

"Lile soko ilikuwa mvua ikinyesha kuna tope, nilienda kipindi hicho, nikajichanganya kumpa mtu mzigo wangu, nilijuta,” amesema Majura.

"Alikuwa hajali matope, alipita popote ili nisimpoteze nikalazimika na mimi kumfuata, asinipotee, nilijuta."

Polisi wafuatilia

Ofisi ya Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Ilala ilieleza kutopokea kesi kama hizo.

“Tunashukuru kwa taarifa, lakini ofisi ya RPC haijapokea kesi ya aina hiyo, ila tutalifanyia kazi, ingawa pia kwa hapa Dar es Salaam, msemaji ni mmoja tu, Kamanda Muliro, wasiliana naye,” amesema askari aliyekuwa kwenye ofisi hiyo ambaye hakujitambulisha.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, ACP Jumanne Muliro alipotafutwa amesema hawezi kuzungumza bila takwimu.

“Hata hivyo, kwa wale wanaoibiwa, wanapaswa kutoa taarifa polisi hata kama hawamfahamu aliyewaibia.

“Kwa kesi kama hizo sio lazima umfahamu aliyekuibia, unashtaki tukio na kilichoibwa… ni kama vile watu wavamie usiku nyumbani kwako na kuiba, utashtaki, hivyo hata hilo unashtaki ingawa siwezi kulizungumzia zaidi kwa kuwa sina takwimu,” amesema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live