Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yazuia vifaranga 62,730 vilivyoingizwa nchini kutoka Ubelgiji

Images (19) Vifaranga.jpeg Wizara yazuia vifaranga 62,730 vilivyoingizwa nchini kutoka Ubelgiji

Sat, 24 Dec 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga amesema wamezuia vifaranga 62, 730 vya kuku wa mayai kuingia nchini baada ya kubainika kutokuwa na vibali pamoja na cheti cha afya.

Vifaranga hivyo ambavyo ni mali ya kampuni ya Phoenix Farms Limited ya Mkuranga mkoani Pwani vilivyohifadhiwa katika makasha 697 vilikuwa vinatokea Ubelgiji na vimezuiliwa katika uwanja ndege wa Julius Nyerere eneo la mizigo.

Profesa Nonga amewaambia wanahabari leo Jumamosi Desemba 24, 2022 vifaranga hivyo viliwasili Desemba 22 saa 4 usiku ndipo wakaguzi wa mifugo na mazao yake walipovibaini kwamba vimeingia bila kufuata taratibu na kanuni.

“Kulingana na kifungu cha 54 (2) cha sheria ya magonjwa ya wanyama, sura 156 inakataza kuingiza mifugo na mazao yake nchini bila kuwa na vibali. Kitendo cha Phoenix kutaka kuingiza kuku wa mayai 62,730 ni kukiuka sheria.

“Kanuni ya 26 ya Udhibiti wa Usafirishaji wa Wanyama na Mazao yake GN namba 28/2007 inabainisha kuwa ikiwa wanyama au mazao ya wanyama yatafika nchini bila kibali au cheti cha afya ya wanyama au mazao ya wanyama, mkaguzi aliyeko kituoni azuie uingizaji,” amesema Profesa Nonga.

Profesa Nonga amebainisha kuwa kutokana tafsiri ya vifungu hivyo vifaranga vya kuku wa mayai 62,730 walioletwa na Phoenix Farms Limited wamezuiliwa kuingizwa nchini kwa sababu ni hatarishi.

“Wizara inautaka uongozi wa kampuni hii kuvirudisha vifaranga hivyo Ubelgiji kwa sababu vinaweza kuhatarisha usalama wa kuku nchini, pia waviondoshe katika maeneo ya uwanja wa ndege.

“Zamani vilikuwa vinachomwa moto, lakini sasa hapana bali aliyevileta avirudishe alikovitoa kwa gharama zake,” amesema Profesa Nonga.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live