Wizara ya Madini imezinadi Leseni zipatazo 441 za utafutaji wa madini muhimu na mkakati pamoja na leseni 46 kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo ambazo ni fursa kwa wawekezaji kwa ajili ya kuingia ubia na wamiliki wa leseni hizo kuziendeleza na hatimaye kuanzisha migodi.
Hayo yalibainishwa Novemba 21, 2023 na Kamishna Msaidizi wa Madini kutoka Wizara ya Madini, Mhandisi Ally Samaje wakati akitoa wasilisho la wizara katika Siku ya kwanza ya Jukwaa la Biashara kati ya nchi ya Uingereza na Tanzania ambapo aliieleza hadhira hiyo kuhusu madini muhimu na mkakati yaliyopo Tanzania, fursa zilizopo katika uwekezaji kwenye madini hayo na mikakati ya Serikali katika kuvutia uwekezaji.
Mhandisi Samaje alisema kati ya leseni hizo, Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) linayo miradi ya utafutaji madini muhimu ya lithium, graphite, rare earth elements na shaba ambayo iko katika hatua mbalimbali za uendelezaji na ambazo wawekezaji wanakaribishwa kushirikiana na STAMICO kuziendeleza kufikia hatua ya uchimbaji kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mbali na miradi ya STAMICO, Mhandisi Samaje aliyataja baadhi ya madini muhimu na mkakati katika jukwaa hilo lenye lengo la kukuza ushirikiano wa kikanda na kuwavutia wawekezaji kuwekeza Tanzania katika sekta mbalimbali ikiwemo sekta ya madini kuwa ni pamoja na madini ya lithium, graphite, iron, nickel, phosphate, rare earth element (REE), cobalt na shaba.
Aliongeza kwamba, moja ya mikakati ya Serikali katika kuendeleza madini muhimu nchini ni pamoja na kupata taarifa za kina za kijiolojia kwa kufanya utafiti wa kina kwa kutumia ndege (High Resolution Airborne Geophysical Survey) mpaka kufikia takribani asilimia 50 ya ukubwa wa nchi ifikapo mwaka 2030 hatua ambayo itavutia uwekezaji nchini hususan katika hatua ya utafutaji wa madini mbalimbali.