Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yawezesha vijana ufugaji kuku

KUKU Wizara yawezesha vijana ufugaji kuku

Sat, 25 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WIZARA ya Mifugo na Uvuvi, imetoa vifaranga vya kuku 540 kwa kikundi cha vijana wajasiriamali, ili kuhamasisha ufugaji utakaosaidia kuziba pengo la uhaba wa nyama ifikapo mwaka 2022 pamoja na kukuza sekta ya kuku nchini.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi wa Mazao ya Mifugo na Usalama wa Chakula na Lishe wa wizara hiyo, Gabriel Bura, alikabidhi vifaranga hivyo mwishoni mwa wiki kwa wawakilishi wa kikundi cha vijana watatu wajasiriamali jijini Dar es Salaam.

Bura alisema hatua hiyo inatokana na mkutano uliofanyika kati ya Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo, Prof. Elisante Ole Gabriel na wadau wa tasnia ya kuku uliofanyika Machi 7, mwaka huu.

Kwa mujibu wa Bura, Prof. Gabriel alishawishika na uwapo wa vijana wenye umri wa chini ya miaka 35 walioonyesha nia ya kuwekeza katika tasnia ya ufugaji wa kuku.

Alisema vijana hao wameonyesha uthubutu na wameonekana kupenda tasnia hiyo ili kukabiliana na hali halisi ya soko la ajira, akibainisha kuwa baadhi yao wamesomea fani za sheria na habari na mawasiliano.

Kwa mujibu Bura, mpango kabambe wa miaka 15 wa kuendeleza sekta ya mifugo umeonyesha kuwa kutakuwa na upungufu wa nyama kwa takriban tani 100,000 ifikapo mwaka 2022 kadri kipato cha wananchi kinavyoongezeka.

Alisema wameanza na Mkoa wa Mkoa wa Dar es Salaam na baadaye watakwenda wilayani Mkuranga, mikoa ya Mbeya, Morogoro na Dodoma na kwamba ni mchakato endelevu wa kutoa vifaranga kwa vikundi vya vijana wajasiriamali.

Sarah Urio. msambazaji wa viranga hivyo, aliwapongeza vijana kwa kuonyesha utayari na uthubutu wa kufuga kuku, akisema licha ya vijana hao kupewa vifaranga hivyo, uongozi wa kampuni yake utakuwa bega kwa bega kwa kuwapatia elimu ya namna ya kuendeleza shughuli hiyo ya ufugaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live