Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yaweka wazi uwezo wa NFRA kununua mazao

NFRA Wizara yaweka wazi uwezo wa NFRA kununua mazao

Thu, 30 Apr 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

BUNGE limeelezwa kuwa Wakala wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), kwa sasa una uwezo wa kuhifadhi tani 251,000 nchi nzima.

Kauli hiyo ilitolewa jana bungeni na Wizara ya Kilimo ilipojibu swali la Mbunge wa Nkasi Kusini (CCM), Desderius Mipata.

Katika swali lake, mbunge huyo alisema wananchi wa Mkoa wa Rukwa hususan Jimbo la Nkasi Kusini, ni wakulima wazuri wa zao la mahindi na gharama za uzalishaji wa zao kwa ekari inakadiriwa kufika Sh. 700,000 ambapo mapato ni wastani wa magunia 15-17.

“Serikali kupitia NFRA wametoa bei elekezi ya Sh. 380 kwa kilo bei ambayo haiwezi kurudisha gharama za uzalishaji. Je, ni kigezo gani kinatumika kupanga bei ya zao hili?” Alihoji.

Katika majibu yake kwa mbunge huyo, wizara hiyo ilisema NFRA hununua nafaka chini ya asilimia mbili ya ziada iliyozalishwa nchini.

Awali, ilifafanua kuwa majukumu mahsusi ya NFRA ni kuhakikisha usalama wa chakula kwa kununua na kuhifadhi akiba ya chakula ili kukabiliana na upungufu wa chakula unaoweza kujitokeza nchini kutokana na majanga mbalimbali.

“Kiasi cha nafaka kinachonunuliwa kila msimu kinategemea na nafasi iliyo wazi ghalani, bajeti iliyotengwa kwa ajili ya kununua akiba ya taifa ya chakula pamoja na hali ya uzalishaji wa ziada ya chakula nchini.

"Hivyo, ununuzi wa nafaka hutegemea zaidi sekta binafsi, NFRA huingia sokoni kununua nafaka kama mnunuzi mwingine yeyote katika soko huru," ilisema.

Wizara hiyo ilisema NFRA kama taasisi nyingine au sekta binafsi, hukutana na ushindani wa bei katika ununuzi wa nafaka na hata pale inapofikia hatua ya kuzungusha akiba ya chakula katika masoko.

“Wakati wa kununua akiba ya chakula, NFRA inatumia bei za kununulia mazao kwa kuzingatia bei za soko zinazozingatia ugavi na mahitaji ili kutokuharibu mfumo wa soko na kudhoofisha jitihada za sekta binafsi kushiriki katika biashara ya nafaka nchini.

“Bei iliyotumika katika ununuzi wa msimu wa 2018/19 imezingatia bei za soko katika kununua mahindi, bei hizo pia zilizingatia gharama nyingine ambazo mkulima anazipata katika uzalishaji hivyo kufanya bei zilizotumiwa na wakala kuwa juu zaidi ya wanunuzi wengine wote katika masoko ya Tanzania kwa sasa,” ilisema.

Ilitolea mfano msimu huo kuwa wakala ulinunua mahindi kwa bei ya kati ya Sh. 350 hadi 500 kwa kilo kwa kulingana na hali ya soko katika maeneo husika ya ununuzi.

Ilisema bei hizo ni juu ya wastani wa bei kwa maeneo husika ambao bei za mahindi zimekuwa chini kufikia Sh. 200 na Sh.170 kwa kilo.

“Kigezo kinachotumika ni bei ya soko linalozingatia ugavi wa uzalishaji na mahitaji ya soko na mlaji wa mahindi kwa wakati husika na siyo gharama za uzalishaji,” ilisema.

Ilibainisha kuwa kutokana na wakulima wengine kushindwa kulima kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo, si rahisi kwa NFRA kutumia bei ya kununulia nafaka ambayo itaweza kukidhi matakwa ya kila mkulima.

“Wakati wa utekeleza kazi ya ununuzi, NFRA hulipa ushuru wa mazao (Produce Cess) kwa Mamlaka za Serikali za Mitaa kwa mujibu wa Sheria ya Fedha ya Serikali za Mitaa ya Mwaka 1982,” ilisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live