Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yataja sababu watu kutokula kuku

Ea89c62d75b190d63723f38355094481.png Wizara yataja sababu watu kutokula kuku

Fri, 14 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

WAKATI leo Waislamu wakisherehekea Sikukuu ya Idd el Fitr na kitoweo cha kuku kutarajiwa kutawala milo, serikali imeeleza sababu kadhaa za Watanzania kutokula mazao ya kuku ikiwamo mayai na nyama kuwa ni pamoja na mila na taarifa potofu, kuogopa gharama, hamasa ndogo na watu kudhani ni chakula cha anasa.

Takwimu za Wizara ya Mifugo na Uvuvi zinaonesha kuwa kwa mwaka Mtanzania anakula wastani wa kuku wawili (kilogramu mbili) wakati inapaswa kula kuku 35 kwa mtu kwa mwaka na mayai 300 kwa mtu kwa mwaka.

Akizungumza na HabariLEO katika mahojiano maalumu, Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga, alisema kumekuwa na juhudi za makusudi zinazochukuliwa na serikali kuhamasisha ulaji wa mazao ya kuku, lakini bado ni changamoto.

Profesa Nonga alisema wizara imebaini kuwa sababu zinazowafanya wananchi wengi wasile mazao ya kuku ni hofu ya gharama wakiyaweka mazao hayo kwenye kundi la vyakula vya anasa na mila potofu kwa baadhi ya makabila.

“Kuna makabila kama ndugu zetu Wamasai hawapendi kula kuku wanasema nani ale ndege, wamezoea nyama za mbuzi na ngombe. Wengine wana mila zinazokataza kabila watu wa kundi fulani kula mayai au nyama ya kuku, wengine wanadhani kula kuku na mayai ni anasa kwamba nyama ya kuku inaliwa sikukuu tu,” alisema Profesa Nonga.

Kuhusu mila potofu, gazeti hili lina taarifa za simulizi ya baadhi ya makabila wakiwamo Wachaga, Wamasai na Wapare kuwa wajawazito zamani hawakuruhusiwa kula mayai kwa madai kuwa wakila, mtoto akizaliwa hataota nywele.

Profesa Nonga alisema pamoja na kwamba kuna uhaba wa tani tatu za nyama ya kuku kutokana na uzalishaji kuwa tani 99.7 mwaka 2020/2021 kutoka tani 102 za mwaka 2019/20, lakini mila potofu kama hizo ndio zinachangia kufifisha hamasa ya wananchi kula kuku na mayai na kusababisha watoto kudumaa akili na ukuaji na kuua soko la ndani.

Alisema ulaji wa mazao hayo uko chini akitolea mfano kwa wastani mtu mmoja nchini anakula kilogramu mbili za nyama ya kuku sawa na kuku wawili kwa mwaka wakati kidunia inapaswa ale kuku 35 kwa mwaka kwa nchi za Afrika na kuku 47 kwa nchi za Ulaya na Marekani.

Utafiti wa HabariLEO umebaini kuwa nyama ya ng’ombe na mbuzi ndio ghali zaidi ya nyama ya kuku. Katika maeneo mengi ya miji mikubwa ikiwamo Dar es Salaam, kilogramu moja ya nyama ya ng’ombe ni kati ya Sh 6,500 mpaka 10,000, ya mbuzi ni kati ya Sh 10,000 hadi 15,000 kulingana na eneo huku kuku mmoja wa kisasa kwa maeneo mengi ni kati ya Sh 5,800 hadi 9,000. Aidha, katika maeneo mengi kuku huuzwa kwa vipande.

Kwa upande wa mayai, alisema Shirika la Chakula Duniani (FAO) linaeleza angalau mtu ale mayai 300 kwa mwaka na akiweza ale yai moja kwa siku, lakini kwa nchini, mtu anakula mayai 106 kwa mwaka sawa na yai moja kwa wiki.

Alisema mataifa ya magharini na Asia mtu mmoja anakula mayai 400 kwa mwaka sawa na wastani wa zaidi ya yai moja kwa siku.

Takwimu zinaonesha kuwa mpaka wiki iliyopita nchini kulikuwa na ongezeko la mayai ambako yalikuwa bilioni 4.5 kutoka mayai bilioni 4.05 mwaka 2019/2020 idadi hiyo ikichagizwa na ongezeko la wafugaji wadogo wa kuku wa mayai, nyama na wanaototolesha vifaranga.

Profesa Nonga aliwahamasisha wananchi kupenda kula mazao ya kuku kwani faida zake ni kubwa kiafya na pia ikiwa kila Mtanzania atazingatia ulaji kama inavyopaswa, soko la ndani lenye watu takribani milioni 60 lingeweza kuchochea uchumi wa nchi na kukuza kipato cha wazalishaji wa mazao ya kuku nchini.

Alisema wizara kwa kushirikiana na wadau wa sekta hiyo, wana mipango ya muda mfupi, wa kati na mrefu ikiwamo kuendelea kutoa elimu ili kuhamasisha matumizi ya mazao ya kuku na kuondoa dhana kuwa ni ya gharama kubwa jambo ambalo si la kweli.

Chanzo: www.habarileo.co.tz