Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yasisitiza matumizi ya falsafa ya Kaizen kiuchumi

8b83b8c3032264d7dd3a538a754fbe56 Wizara yasisitiza matumizi ya falsafa ya Kaizen kiuchumi

Fri, 11 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara imewahimiza Watanzania kutumia kwa usahihi Falsafa ya Kaizen ili kuchochea ukuaji wa uchumi na kuvutia wawekezaji.

Aidha, Wizara hiyo imeiomba Serikali ya Japan kupitia kwa Balozi wake nchini, MShinichi Goto, kuendelea kufadhili mradi wa Kaizen ili kusambaza falsafa hiyo kuendana na utekelezaji wa Mpango wa Kitaifa wa Miaka 10 – “FKM 2020-2030”.

Mpango huo umelenga kueneza falsafa ya Kaizen sambamba na kufikia hatua ya kuunganisha magari ya Japan nchini Tanzania.

Akimwakilisha Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Ashatu Kijaji katika ufunguzi wa Maadhimisho ya Tatu ya Siku ya Kaizen Tanzania, Naibu Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Exaud Kigahe, alisema Dar es Salaam jana kuwa, Wizara kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), imekuwa ikitekeleza Mradi wa kuimarisha sekta ya viwanda kupitia falsafa ya Kaizen tangu 2013.

Kaizen ni neno la Kijapan linalomaanisha: “Badilika kwa Ubora/ Uzuri” inahusu shughuli endelevu zinazofanyika ili kuboresha kazi, mifumo, michakato na nyanja yoyote ya kuendesha biashara.

Aliwataka Watanzania kuzingatia ubora na kujikita katika ushindani ili Tanzania isiwe tu soko la bidhaa za nchi nyingine, bali Watanzania washiriki kwa viwango vya ubora wa hali ya juu katika soko likiwamo Eneo Huru la Biashara Afrika.

“Japan na Tanzania ni marafiki, sasa twende zaidi ya hapo; kwa kuwa sisi ndio wateja wenu wakubwa wa magari na Tanzania tumefikia uchumi wa kati. Ni muda mwafaka sasa sekta binafsi ya Tanzania na sekta binafsi ya Japan kufanya uunganishaji wa magari hapa nchini,” alisema Naibu Waziri na kuwasisitiza Watanzania kujiandaa vema kwa hilo kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Akizungumza katika ufunguzi wa maadhimisho hayo yenye Kaulimbiu isemayo: “Kaizen! Kwa Tanzania ya Viwanda na Maendeleo Jumuishi!” Balozi wa Japan nchini Tanzania, MShinichi Goto, alipongeza Tanzania kwa kukua kiuchumi licha ya changamoto zilizotokana na Covid-19.

Alisema nchi za Afrika ikiwamo Tanzania zinapaswa kutilia mkazo maendeleo ya biashara na viwanda vidogo na vya kati ili kukuza uchumi.

Mwakilishi Mkazi Mkuu wa JICA nchini Tanzania, Yamamura Naofumi, alisema tangu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara na JICA zishirikiane kutekeleza falsafa ya Kaizen, mwaka 2013, zaidi ya kampuni 100 nchini zinatekeleza falsafa hiyo na Watanzania 150 wamefuzu kuwa wakufunzi wa Kaizen.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live