Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara yapewa somo kusaka masoko ya mazao

49512 Pic+mazao Wizara yapewa somo kusaka masoko ya mazao

Mon, 22 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WIZARA ya Kilimo imeshauriwa kuanzisha kitengo maalum cha kutafuta masoko kwa ajili ya mazao ambayo wakulima wanahamasishwa kuzalisha ili kuepuka mazao hayo kukosa soko na wakulima kuingia hasara.

Ushauri huo ulitolewa mwishoni mwa wiki na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Alibert Chalamila, alipokuwa anafungua mkutano wa asasi ya Uwezeshaji wa Sekta Binafsi ya Kilimo (Pass Trust) na wadau wa kilimo, mifugo na uvuvi.

Pass iliitisha mkutano huo kwa ajili ya kuwaeleza wadau hao wakiwamo wakulima na wadau wengine wanaohusika kwenye mnyororo nwa thamani wa mazao ya kilimo kuhusu fursa ya upatikanaji wa mikopo kwenye sekta ya kilimo.

Chalamila alisema Wizara ya Kilimo imekuwa ikiwahamasisha wakulima kuzalisha mazao mbalimbali kwa wingi, lakini utafutaji wa masoko inaachiwa Wizara ya Viwanda na Biashara, hali ambayo inapunguza ufanisi wa upatikanaji wa masoko.

Alisema ili kuhakikisha wakulima wananufaika na kile wanachozalisha, ni lazima Wizara ya Kilimo ikaanzisha kitengo ambacho kitakuwa kinashirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara kutafuta masoko ya mazao mbalimbali ya wakulima.

“Sasa hivi tunahimiza zaidi vijana kujiajiri na wengi wao wanajiajiri kwenye kilimo na Wizara inatumia nguvu kubwa kuhamasisha uzalishaji, lakini utafutaji wa masoko inakuwa tatizo, sasa ni vema uhamasishaji ukaenda sambamba na utafutaji wa masoko,” alisema Chalamila.

Aliipongeza Pass Trust kwa juhudi zake za kuwasaidia wakulima kupata mikopo kutoka kwenye taasisi mbalimbali za fedha inayowasaidia kuongeza uzalishaji na kwamba hali hiyo imeongeza usalama wa chakula nchini.

Awali akitoa taarifa ya utoaji wa mikopo, Mkurugenzi Mtendaji wa Pass Trust, Nicomed Bohay, alisema taasisi hiyo ilisajiliwa rasmi mwaka 2007 na kwamba mpaka sasa imewasaidia Watanzania 1,200,000 kupata mikopo yenye thamani ya Sh. bilioni 916.

Alisema taasisi hiyo inafanya kazi ya kuwaunganisha wakulima na taasisi za fedha pamoja na kuwadhamini kupata mikopo ya kuendeleza kilimo ili kuinua uchumi wao na wa taifa.

“Serikali iliamua kuiendeleza taasisi hii kutokana na kwamba inatambua kuwa Sekta binafsi ndio injini ya uchumi, tunachokifanya ni kuwasaidia wakulima na wadau wengine wanaoshiriki kwenye mnyororo wa thamani kwenye mazao ya kilimo kupata mikopo,” alisema Bohay.

Alisema kwenye mkutano huo walishiriki wadau mbalimbali wakiwamo wakulima, waagizaji wa mbolea, wauzaji wa pembejeo, wanunuzi wa mazao ya wakulima, wasindikaji wa mazao, wauzaji wa zana za kilimo na wawakilishi wa benki zote zinazoshirikiana na Pass Trust.

Kwa upande wake, Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Uzalishaji wa Mkoa wa Mbeya, Said Madito, alisema mikopo ambayo wakulima wanaipata inasaidia kukuza uzalishaji wa mazao yao na kuinua kipato chao.

Aliwataka wadau wote wanaosaidiwa kupata mikopo hiyo kuwa waaminifu kwenye urejeshaji wa mikopo hiyo pamoja na kuhakikisha wanaitumia mikopo hiyo kwa malengo wanayokusudia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live