Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara ya Utalii yaweka mikakati kuzuia uhalifu

8a991d826cd3652493e520bf98b8295f Wizara ya Utalii yaweka mikakati kuzuia uhalifu

Mon, 4 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wizara ya Maliasili na Utalii, imesema itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia ofisi za upelelezi za mikoa na wilaya katika kushughulikia masuala yote yanayohusu uhalifu wa wanyamapori na mazao ya misitu.

Kauli hiyo ilitolewa jana mkoani Singida na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma Mkomi, wakati akifungua kikao kazi cha wizara kilichowahusisha Wakuu wa Upelelezi wa Mikoa (RCO), Makamishina wa Uhifadhi na Wakuu wa Kanda wa Jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori na Misitu (JU).

‘’Ni matumani yangu mtatumia mjumuiko huu vizuri, ili ninyi wenzetu muweze kutusaidia namna bora ya kuwezesha kuliimarisha jeshi letu pamoja na kukuza ushirikiano baina ya Jeshi la Uhifadhi na Jeshi la Polisi,’’ amesema.

Amesema kuwa wizara katika kutekeleza jukumu lake la uhifadhi wa rasilimali za wanyamapori na misitu, ikiwa katika mfumo wa kiraia, ilikutana na changamoto mbalimbali, hali iliyoilazimu kubadili mfumo wa utendaji kazi wa taasisi 4 za uhifadhi.

Taasisi hizo ni Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA), Shirika la Hifadhi (TANAPA), Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA) na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), kuingia rasmi kwenye mfumo wa kijeshi.

Naibu Katibu Mkuu Juma Mkomi, amezitaja baadhi ya changamoto zilizokuwepo ni pamoja na ugumu wa upatikanaji wa vitendea kazi, ujangili wa kutumia silaha za kivita na ucheleweshwaji wa ushughulikiaji mashauri ya kinidhamu kwa watumishi na kukosekana kwa mnyororo wa utoaji amri.

Amelipongeza Jeshi la Polisi kwa namna ambavyo limekuwa likishirikiana na Wizara ya Maliasili na Utalii kupambana na ujangili wa Wanyamapori na Mazao ya Misitu, kabla na baada ya kuanzishwa Jeshi la Uhifadhi.

‘’Wizara imeendelea kuwajengea uwezo maofisa na askari kwa kuwapelekea kozi mbalimbali, hususan za ukusanyaji taarifa, uchunguzi pamoja na uendeshaji wa Mashitaka.

“Mpaka sasa idadi ya maofisa na askari ambao wameshapata mafunzo bado ni ndogo, ikilinganishwa na ukubwa wa maeneo ya kiutendaji,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live