Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara ya Maji yafungua milango uwekezaji sekta binafsi

Maji Wizara ya Maji yafungua milango uwekezaji sekta binafsi

Tue, 28 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali kupitia Wizara ya Maji imesema imefungua fursa ya kuingia ubia wa mashirika ya sekta binafsi na umma (PPT) kuboresha upatikanaji wa huduma ya maji kwa wananchi mijini na vijijini.

Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema leo, Novemba 27,2023 wakati akifungua kongamano la maji la mwaka 2023 lililiandaliwa na Umoja wa Wasambazaji Maji Tanzania (ATAWAS).

Mhandisi Mahundi amesema uamuzi huo ni utekelezaji wa maudhuhi ya sera ya Taifa ya mwaka 2002 iliyohimiza ushirikiano wa sekta ya umma na binafsi, ili kuboresha huduma za maji mijini na vijijini.

“Nchi yetu ina jumla ya vijiji 12,318 ambapo vijijij 9, 670 vimefikiwa na huduma ya maji, sawa na asilimia 77 huku kwa mijini ikiwa ni wastani wa asilimia 88 pekee,” amesema.

“Malengo ya Serikali ni kutekeleza ilani ya uchaguzi 2020 kwa kuhakikisha wananchi waishio vijijini wanafikiwa na huduma ya maji kwa asilimia 85, huku asilimia 95 mijini ifikapo 2025,”amesema.

Amesema wizara imekuwa ikifanya juhudi kwa kushirikiana na sekta binafsi kuboresha huduma za maji, ikiwepo utunzaji vyanzo vya maji, uzalishaji, usambazaji na utawala wa fedha.

“Mwaka 2018 Wizara ya Maji na Umwagiliaji kwa kushirikiana na Wizara ya Viwanda na Biashara, wadau wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo, waliingia makubaliano ya namna bora ya kuchangia kuboresha huduma ya maji nchini,” amesema.

Mhandisi Mahundi amesema hatua hiyo imewezesha kutengeneza mpango kazi wa miaka mitano kuanzia mwaka 2018/23 wa kuboresha dawati la ubia kuratibu miradi mitano kati ya sekta ya umma na binafsi nchini.

Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Sera, Mipango, Utafiti na Ubunifu, Wizara ya Maji, Alex Tarimo amesema sekta binafsi zifanye tathimini ya hali ya upatikanaji wa huduma za maji mijini na vijijini na kuwasilisha mrejesho wizarani.

“Lengo ni kuona Watanzania wanafikiwa na huduma za msingi, sambamba na kudhibiti upotevu wa rasilimali za maji safi na salama na kuwezesha sekta ya maji kufanya vizuri zaidi,”amesema.

Ofisa Uhusiano na Mawasiliano wa Chuo cha Maji, Ghamina Charles amesema wanakuja na mfumo wa teknolojia ya kisasa ya kubaini utendaji kazi wa wasoma mita ili kudhibiti malalamiko ya wateja kubambikiziwa ankara za maji.

“Mfumo huo utasaidia taasisi kubaini maeneo ya wateja waliosomewa taarifa za matumizi ya maji na maeneo ambayo hawajapita wasoma mita, hali ambayo itasaidia uhalali wa malipo ya wateja baada ya kupata huduma,”amesema.

Mwenyekiti wa Umoja wa Wasambazaji Maji Tanzania (ATAWAS), Geofrey Hilly amesema lengo la kongamano hilo ni kuboresha huduma ya maji safi kwa Watanzania, ili kufikia mipango mikakati ya nchi za Afrika na duniani ifikapo 2030.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live