Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara mbili kikaangoni kuzota kwa biashara nchini

686a037c7cb91f75482ab0929f61f1be Wizara mbili kikaangoni kuzorta kwa biashara nchini

Tue, 2 Aug 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango ameiagiza Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara ishirikiane na Wizara ya Fedha na Mipango kubaini sababu za wafanyabiashara nchini kuhamishia biashara zao nchi jirani.

Dk Mpango ameagiza wizara hizo zishirikiane na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Bodi ya Biashara ya Nje kubaini ukubwa wa tatizo hilo. Alisema hayo jana wakati akifungua maonesho ya kilimo ya Nanenane kitaifa katika viwanja vya John Mwakangale mkoani Mbeya.

Dk Mpango alisema amepata taarifa ya kushuka biashara kati ya Tanzania na nchi jirani katika ukanda wa Nyanda za Juu Kusini licha ya kuwepo bandari inayowezesha kupata bidhaa kwa gharama nafuu na pia Benki Kuu Tanzania (BoT) kupunguza gharama na kurahisisha ubadilishanaji bidhaa mipakani.

“Lakini pia nimeambiwa baadhi ya wafanyabiashara wa nchi jirani wanapitishia bidhaa katika nchi nyingine badala ya moja kwa moja kutoka hapa Tanzania. Kwa hiyo ninawataka wizara nilizozisema mbaini kiini cha tatizo hili na mtafute ufumbuzi mara moja,” alisema.

Dk Mpango aliagiza wizara hizo na taasisi zake wazungumze pia na wafanyabiashara Watanzania walioamua kuhamia Zambia au Malawi kuhusu tatizo hilo. Alipiga marufuku gunia la lumbesa kutumika katika mikoa yote na akaagiza wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya wasimamie hilo.

Dk Mpango aliagiza halmashauri ziache kutumia lumbesa kama chanzo cha mapato na akaagiza kuanzia sasa mazao ya wakulima yapimwe kwa kilo na si kupitia magunia yasiyotoa vipimo hivyo kuwapunja wakulima.

Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe alisema lumbesa limeendelea kuwa kansa kwani licha ya kuzieleza hadi kuziandikia barua halmashauri kukomesha kifungashio hicho lakini lumbesa zinatumika.

Bashe alisema wafanyabiashara wanaotumia lumbesa wanapopigwa faini na halmashauri ambayo huona hatua hiyo ni kuongeza mapato, wafanyabiashara hulipa na kuendelea kutumia lumbesa kwa sababu faini ni ndogo kuliko faida wanayopata.

Alisema kama mikoa yote haitapiga marufuku lumbesa litaendelea kutumika kwa kuwa uzoefu uliopo ni kwamba mkoa mmoja unapopiga marufuku, wafanyabiashara wanakimbilia mkoa mwingine ambako lumbesa linaendelea kutumika.

Dk Mpango pia aliagiza mifugo katika minada ianze kuuzwa kwa kupimwa kwa kilo na si kwa kukadiria kwa kuangalia umbo. Mapema wakati anazunguka katika mabanda, Dk Mpango alielezwa kwamba kwa sasa bei ya ng’ombe ni wastani wa Sh 3,500 kwa kilo (kabla hajachinjwa).

Dk Mpango alizitaka halmashauri zitenge bajeti ya kuwezesha maofisa ugani kuwafikia wananchi na wasikae ofisini na ni lazima kila ofisa ugani awe na shamba darasa.

Alizitaka ofisi za utafiti wa kilimo kuibua mbegu bora na kuzisambaza na kuzijaribu katika kila mkoa. Alizitaka taasisi kama ya Utafiti wa Mazao ya Kilimo (TARI) na Wakala wa Mbegu za Kilimo (ASA) zilete mabadiliko katika kilimo kwa kuwa katika bajeti ya mwaka huu wa fedha, Tari imeongezewa bajeti kutoka Sh bilioni 11 mwaka 2021/22 hadi Sh bilioni 40.13 wakati ASA imeongezewa bajeti kutoka Sh bilioni 5 hadi Sh bilioni 43.7.

Dk Mpango aliagiza kuwe na soko la uhakika la mazao ya wakulima hivyo wizara za kisekta zitafute masomo hayo ndani na nje ya nchi lakini mazao yauzwe kwa tahadhari.

Awali wakati anatembelea mabanda aliitaka Wizara ya Kilimo itoe changamoto kwa maprofesa wa kilimo wawekeze kwenye sekta hiyo badala ya kujenga gesti na baa.

Alisema kilimo kinalipa na kama maprofesa wa kilimo hawawekezi kwenye sekta hiyo wananchi wengine hawatavutika kuwekeza huko.

Dk Mpango alimuagiza Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe aende kutoa changamoto hiyo kwa maprofesa wa kilimo katika Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine, Morogoro.

Pia aliiagiza wizara hiyo ione namna ya kutoa bima ya kilimo kwa wananchi ili wasiendelee kupata hasara kutokana na changamoto mbalimbali

Chanzo: www.tanzaniaweb.live