Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wizara, JICA wajipanga usambazaji Gesi asilia

Gesi Urusii.jpeg Wizara, JICA wajipanga usambazaji Gesi asilia

Sat, 28 Oct 2023 Chanzo: Mwananchi

Viongozi wa Wizara ya Nishati pamoja na ujumbe wa Wataalam kutoka Shirika la Maendeleo la Japan – JICA, wamefanya kikao kazi kuhusu utekelezaji wa mradi wa kujengea uwezo Wizara ya Nishati, Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania – TPDC na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji – EWURA, katika masuala ya kusanifu mitandao ya usambazaji wa Gesi Asilia.

Akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Mkurugenzi wa Sera na Mipango, Petro Lyatuu alisema kuwa, mradi huo kwa upande wa Tanzania una umuhimu mkubwa kwani utasaidia matumizi ya uhakika ya Gesi Asilia.

Almesema, faida za mradi huo ambazo ni pamoja na kuongeza utalaam kwa wazawa kutokana na mafunzo mbalimbali yatakayotolewa katika masuala ya kuendesha miradi ya Gesi Asilia nchini ambapo nchi itaongeza pia idadi ya watalaam kutokana na mafunzo hayo.

Lyatuu aliongeza kuwa, katika kipindi hiki ambacho nchi ipo kwenye mkakati wa kuingia katika matumizi ya nishati safi ya kupikia, mradi huo wa kuwajengea uwezo wataalam katika masuala ya Gesi Asilia utasaidia pia katika kutekeleza mkakati huo.

Kwa upande wake, Mwakilishi Mkuu wa JICA Ofisi ya Tanzania, Hitoshi Ara, aliishukuru Wizara kwa ushirikiano waliotoa kutoka mwanzo wa makubaliano ya utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa Shirika hilo litaendelea kutoa ushirikiano kwa Wizara pale itakapohitajika.

Mradi huo wa kusanifu mitandao ya Gesi Asilia unahusisha Mkoa wa Dodoma, Pwani na Dar es Salaam na katika kikao hicho ilitambulishwa rasmi timu ya Wataalamu watakaohusika na mradi huo pamoja na kujadili majukumu ya kila upande katika utekelezaji wa Mradi husika.

Chanzo: Mwananchi