Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) tawi la Shinyanga umezindua wiki ya huduma kwa wateja katika kuhakikisha linaboresha utoaji wa huduma na kuimarisha uhusiano kwa wateja.
Ufunguzi wa wiki ya huduma kwa wateja ukiongozwa na kauli mbiu ya "Ushirikiano kwa huduma bora", umefanyika leo Oktoba 02, 2023 katika ofisi za Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) Mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza wakati wa ufunguzi huo Meneja wa NSSF Mkoa wa Shinyanga Amina Mdabi amewashukuru wateja kwa kuendelea kushirikiana vyema na kuiamini NSSF na kujiunga huku akiahidi kuwa NSSF itaendelea kutoa huduma kwa ufanisi na kuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya rushwa.
"Niwapongeze watumishi wote kwa ujumla kwa juhudi kubwa za pamoja mnazozifanya katika kuwahudumia wateja wetu, mfuko unatambua mchango wenu katika kutekeleza majukumu mliyonayo naomba muendelee kufanya kazi kwa uadilifu na kuepuka vitendo vya rushwa ambayo ni kero na inadumaza maendeleo katika jamii," amesema Mdabi.
Nao baadhi ya wanufaika wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) mkoa wa Shinyanga waliojitokeza kwenye ufunguzi huo akiwemo Dorica Bushu na John Ndama wamesema wanaishukuru NSSF kwa kuendelea kuwajali kupitia huduma mbalimbali wanazozitoa kupitia mfuko wa taifa wa hifadhi ya jamii.