Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wiki mbili maonyesho ya Sabasaba kidigitali zaja

64856 Bashungwa+pic Wiki mbili maonyesho ya Sabasaba kidigitali zaja

Mon, 8 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAONYESHO ya 44 ya Kimataifa ya Biashara Dar es Salaam (DITF), yanatarajia kuanza Julai Mosi hadi 13 mwaka huu, katika Uwanya wa Maonyesho wa Julius Nyerere.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa, uratibu wa maonyesho hayo unazingatia kanuni za afya kwa lengo la kuchukua hatua za kujikinga na maambukizo ya corona.

Ilielezwa kuwa mikutano ya ana kwa ana ya wafanyabiashara (B2B) mwaka huu itaandaliwa na kuratibiwa kwa njia ya mtandao.

Pia, watembeleaji watakuwa wananunua tiketi kupitia simu za mikononi, huku watembeleaji wengine wa ndani na nje ya nchi wakipewa fursa kufuatilia maonyesho hayo kupitia mitandao itakayokuwa inarusha moja kwa moja.

“Uratibu wa maonyesho unazingatia kanuni za afya kwa lengo la kuhakikisha kuwa uwanja wa maonyesho unakuwa salama kwa waonyeshaji na watembeaji kwa kuchukua hatua stahiki za kujikinga na maambukizo ya Covid-19,” alisema Bashungwa katika taarifa yake hiyo.

“Ili kurahisisha, watembeleaji wa maonyesho watapata fursa ya kununua tiketi kupitia simu za mikononi, watembeleaji kutoka ndani na nje ya nchi watapata fursa ya kutembelea maonyesho hayo kupitia mitandao na kutakuwa banda maalum la kutangaza bidhaa za kilimo yakiwamo mazao ya kimkakati," aliongeza.

Waziri Bashungwa alitoa wito kwa wafanyabiashara, wamiliki wa viwanda vyote nchini, wakulima, taasisi za umma, halmashauri za wilaya na taasisi binafsi, kushiriki katika maonyesho hayo ili kuongeza wigo wa masoko ya kilimo, viwanda, mifugo, uvuvi na madini.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live