Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye mabwawa ya tope sumu watahadharishwa El Nino

Mvua Yawatenga Wananchi Wa Kata Ya Maboga Na Wengine Wenye mabwawa ya tope sumu watahadharishwa El Nino

Wed, 29 Nov 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali imewataka wamiliki wa mabwawa ya tope sumu yaliyopo migodini kuchukua tahadhari za mvua za El Nino kwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara kuepusha athari endapo mabwawa hayo yatabomolewa na mvua hizo.

Akizungumza mara baada ya kufungua mafunzo ya kuangalia usalama na teknolojia ya mabwawa ya maji na mabwawa ya tope sumu leo Jumanne Novemba 28, 2023; Mkurugenzi Rasilimali za Maji kutoka Wizara ya Maji, Dk George Lugomela amesema kipindi hiki cha mvua mmiliki lazima ahakikishe bwawa lake lipo salama.

“Kingine ni kuhakikisha kwamba pale panapokuwa na ule uchochoro wa maji panakuwa safi ili maji yakizidi yaweze kutoka. Kwa yale mabwawa makubwa kabisa ambayo yana mageti ya kufungulia maji wahakikishe kwamba hawasubiri mpaka bwawa lijae sana ndio wafungulie,

“sababu maji yanakuja kwa wingi…wafungulie haraka sana yasilete athari kwa watu, viumbe hai na mazingira,”amesema Dk Lugomela

Katibu Mtendaji wa Chemba ya Migodi Tanzania, Mhandisi Benjamin Mchwampaka amesema endapo kama utunzwaji wa mabwawa hayo si mzuri yanaweza kubomoka huku akiwataka kutumia teknolojia kujua viashiria vya hatari nakuchukua hatua kabla ya madhara.

“Mabwawa haya yanatunza vitu vingi na endapo kama hayafuatiliwi vizuri au utunzaji wake sio mzuri yanaweza kubomoka hasa kipindi hiki cha El nino mvua ikinyesha kwa wingi yanaweza kubomoka na kuleta madhara makubwa kwa wananchi wanaoishi chini ya hilo bwawa na pia kuchafua ardhi,”amesema

“Kwahiyo ndio maana kwenye haya mafunzo kuna wataalamu kutoka Afrika Kusini na Ispania… wataalamu hawa wamekuja ili watuambie ama kutushauri kuwa jamani teknolojia ambazo zipo sokoni ni hizi na zipi tunapaswa tuzitumie ili mmiliki wa mgodi au yule mwangalizi wa madini kuchagua teknolojia bora na nzuri zaidi,”ameongeza

Mhandisi muelekezi ambaye pia ni Mwenyekiti wa kamati ya usalama mahala pa kazi na mazingira kutoka Chemba ya Migodi, Anael Macha amesema mabwawa yote yanatakiwa yasanifiwe kabla ya kujengwa kama hadidu za rejea zilivotengenezwa kutokana na uzalishaji au aina ya tope sumu iliyopo kwenye eneo la uchenjuaji.

“Taratibu zote za kihandisi lazima zizingatiwe, mambo yote kabla ya ujenzi wa lile bwawa kama vile kiasi cha mvua au kiasi cha maji kitakachopokewa kutokana na uzalishaji, aina ya udongo utakaotumika kwa ajili ya kujenga lakini pia lazima uzingatie mitetemeko inayoweza kutokea katika hayo maeneo,”

“Kufanya huo usanifu inatakiwa upitishwe kwenye Mamlaka za Kiserikali ili ziweze kuthibitishwa ubora wake kama unaweza kuhimili,”amesema

Amesema moja ya vigezo vya kuzingatia wakati wa kutengeneza bwawa la tope sumu nikuangalia kiwango cha mvua na mara nyingi wanachukua historia ya mvua ya zaidi ya miaka 20

“Bila shaka utaona mvua zinazonyesha leo zimewahi kunyesha miaka 20 iliyopita au miaka 15 kwahiyo kama bwawa limezingatia vigezo vyote vya kiuhandisi basi hizi mvua hazitakuwa na tatizo,

“Lakini kama hazikuzingatia zinaweza kubadilika kuwa tope au uji uji na hatimaye kumwagika kama zile kingo hazitaweza kuhimili na madhara yanaweza kuwa makubwa sana ya papo kwa papo kama vile kifo na madhara ya baadaye kama magonjwa ya Saratani,”amesema Macha

Warsha hiyo imeandaliwa na Wizara ya Maji kwa kushirikiana na Chemba ya Migodi nchini ili kutoa mafunzo kwa wataalamu mbalimbali wanaohusika na usimamizi wa usalama wa mabwawa wakiwemo wamiliki wa mabwawa, wataalamu wa mabwawa, wasimamizi wa mabwawa, Baraza la Taifa la Usimamizi wa Mazingira (NEMC), Tume ya Madini pamoja na wadau wengine.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live