Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye mabucha ya nyama pori wapewa mbinu

A73635fa18a06ddb665cbcb09012d335 Wenye mabucha ya nyama pori wapewa mbinu

Wed, 3 Feb 2021 Chanzo: habarileo.co.tz

NAIBU Kamishna wa Utalii na Huduma za Biashara kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa), Imani Nkuwi amesema baadhi ya wenye mabucha ya nyamapori waliopewa leseni za uuzaji nyama hiyo hawakufanya tafiti juu ya upatikanaji wa wanyama pori.

Aidha, wauzaji wa nyama hizo wameiomba serikali kurudisha utaratibu wa uwindaji katika vitalu kila wilaya ili kuwezesha nyama hizo kupatikana kwa wingi katika mabucha ya nyama hizo.

Akizungumza mjini hapa jana kwenye warsha ya siku tatu iliyowashirikisha wadau wa nyama pori kutoka mikoa mbalimbali nchini, Nkuwi aliwasihi wauzaji hao kufanya tafiti zaidi pamoja na kutii sheria za uwindaji wanyama pori.

“Serikali imeanzisha bucha za wanyamapori kwa lengo la kupunguza ujangili wa wanyama, lakini pia ni lazima ukitaka kuwinda ufanye utafiti ili kubaini mbinu za kupata wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa,” alisema.

Nkuwi alisema baada ya kufanya uzinduzi wa bucha ya nyama jijini Dodoma Desemba, mwaka jana, Tawa imekuwa ikipata malalamiko mengi ya wafanyabiashara waliopewa leseni kutokuwa na uzoefu wa biashara hiyo.

"Lazima unapotaka kuwinda ufanye utafiti kwanza na ujue aina za wanyama wanaoruhusiwa kuwindwa na upigaji wake na ndio maana tumekutana hapa kwa ajili ya kujadili changamoto wanazokumbana nazo katika kuanzisha mabucha ya nyama pori," alisema.

Alisema Tawa awali ilipokea maombi 55 ya leseni za uwindaji wanyamapori kutoka mikoa 16 na kati yake maombi 46 kutoka mikoa 14 yalikubaliwa na kuanza kazi.

"Uwindaji ni utafutaji na vile vyanzo vinavyohusisha uwindaji ni lazima viheshimiwe na kuna vibali vya siku siku 10, 14 hadi 21, lakini kuna watu katika uwindaji wanakata tamaa kutokana kukosa, hivyo zingatieni sheria, kanuni na taratibu huku mkizingatia mipango yenu ya biashara,” alisema.

Awali, baadhi ya wadau wa nyamapori, mratibu wa bucha za wanyamapori Tanzania, Emmanuel Absalom na Hillary Daffi waliomba Tawa kuongeza maeneo ya uwindaji kwani kati ya 10 yaliyotengwa hivi sasa sita hayafanyi kazi, huku manne uwindaji wa wanyama ukisuasua.

Absalom alisema mashamba pori nayo yanahitaji miaka mitatu au minne kupata nyama ndio maana baadhi ya mabucha ya nyamapori yanakosa nyama kutokana ba changamoto hizo za uwindaji.

Aliomba serikali kufunga vitalu vya uwindaji kila wilaya ili nyama zipatikane kwa wingi na wananchi wanunue na kuzila.

Alidai vitalu walivyopewa kuwinda wanyama havina wanyama na vitalu vingine havifikiki kutokana na mvua zinazonyesha hivi sasa na kusababisha magari ya uwindaji kukwama.

Chanzo: habarileo.co.tz