Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Wenye mabenki watoa sababu za kutokopesha wachimbaji madini

37833 Pic+mabenki Wenye mabenki watoa sababu za kutokopesha wachimbaji madini

Tue, 22 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa umoja wa mabenki Tanzania, Abdulmajid Nsekela amesema benki zimekuwa zikishindwa kutoa mikopo kwa wachimbaji wadogo kutokana na ukosefu wa leseni na wengine kukodisha jambo ambalo linawafanya washindwe kutambua uhalali wao.

Nsekela ambaye pia ni mkurugenzi mtendaji wa benki ya CRDB amesema hayo leo katika mkutano wa wachimbaji, wafanyabiashara na wadau wa sekta ya madini nchini unaofanyika jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais John Magufuli.

 “Wachimbaji hao wamekuwa wakishindwa kufanya upembuzi yakinifu wa mapato yao ambao husaidia benki kutathimini wanachozalisha ili waweze kukopeshwa.”

“Wamekosa mshikamano na umoja ambao ukitiliwa mkazo utaleta matokeo chanya lakini pia wamekuwa wakihamahama jambo ambalo huweka ugumu kwa mabenki kufuatilia utendaji wao,” amesema.

Amesema  kutokana na idadi ya benki kuongezeka amana pia imeongezeka hadi kufikia Sh29.9 trilioni kutoka Sh19.5 trilioni mwaka 2013 hivyo kuwezesha benki hizo kuendelea kufanya vizuri.

Amesema kutokana na kabadilika kwa sera za uendeshaji wa benki hizi sasa watajikita zaidi katika shughuli za kiuchumi na sekta ya madini.

“Mabenki yamekuwa yakishiriki katika sekta ya madini katika njia mbalimbali ikiwamo kutoa mikopo kwa wachimbaji mmoja mmoja na wakandarasi na kushiriki katika shughuli mbalimbali,” amesema

“Salio la mikopo iliyotolewa limezidi kukua kutoka Sh306 bilioni 2016 hadi kufikia Sh357 bilioni katika mwaka 2018 huku makubaliano yakiwa ni kupelekwa katika shughuli za madini tu,” amesema.

Amesema uzalishaji wa wachimbaji wadogo umekuwa duni kwa muda mrefu kutokana na kukosa nyenzo, mitaji jambo ambalo limefanya washindwe kutoa mchango unaostahili.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz