ZAIDI ya Sh bilioni 196 zinapotezwa na wasafirishaji wa mabasi kila mwaka kutokana na kutotumia mfumo wa ukatishaji tiketi kwa njia ya mtandao (POS) uliobuniwa maalumu kwa utoaji wa huduma ya usafiri.
Aidha hatua hiyo pia imekuwa ikiipotezea serikali zaidi ya Sh bilioni 38 kila mwaka zinazotokana na kodi endapo wasafirishaji hao wangetumia mfumo huo .
Hayo yalibainishwa na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Dk Edwin Mhede wakati wa mkutano wa wadau mbalimbali kutoka sekta ya usafirishaji nchini uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Katika mkutano huo uliohudhuriwa na Mamlaka ya Udhibiti wa usafiri Ardhini (LATRA), Dk Mhede alisema umefika muda muafaka kwa wasafirishaji hao kutumia mfumo huo ili kujitengezea fadia na hivyo kukuza uchumi wao.
" Kuna fadia nyingi sana kutumia mfumo huu, mbali na faida inayotokana na utumiaji wake, pia inalinda usalama wa chombo kwa kumfanya mmiliki kufuatilia mwenendo wa safari zake" alisema Dk Mhede.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa LATRA, Gilliard Ngewe mbali na kusisitiza wasafirishaji wa mabasi kuingia katika mfumo huo, ni muhimu kwa kipindi hiki kwa wasafirishaji hao kutumia POS kwa kuwa unarahisisha shughuli nzima ya utoaji huduma.
Alisema LATRA kama msimamizi wa huduma za usafiri ardhini inawataka wasafirishaji hao kuingia katika mfumo huo kutokana na kuwa na manufaa wa wasafirishaji pamoja na wasafiri nchini kote.
Chama cha Wamiliki wa Mabasi Tanzania(TABOA)kupitia kwa Mweka Hazina wake, Issa Nkya, kimesema wao kama wasafirishaji hawana tatizo la kuingia katika mfumo huo isipokuwa kinachotakiwa wapewe elimu ya kutosha juu ya utumiaji wa mfumo huo.
Alisema Taboa na wanachama wake wote wapo tayari kutumia mfumo huo wakati wowote watakapokuwa wamepewa elimu ya namna ya kuutumia huku akisisitiza kuwa lengo ni kuunga mkono juhudi hizo za serikali.