Wafanyabiashara wa nyumba za kulala wageni mkoani Geita, wameiomba serikali kupitia upya mapendekezo ya kodi mpya ya asilimia 1 ya kitanda wanayotakiwa kulipa kila mwezi kwani kodi zinazidi kuwa nyingi hali inayoweza kupelekea kufunga biashara zao.
Wakiongea mara baada ya kumalizika kwa semina ya tozo hiyo baadhi ya wafanyabiashara wameiomba serikali iweze kuwaondolea hiyo tozo kwani inaongeza mzigo kwa wamiliki wa nyumba hizo.
"Tozo hizi za bed night levy, ukweli zinaleta mkanganyiko kulingana kwamba TRA ina tozo nyingine ambayo ni aslimia 18 ya VAT, hivyo basi tukawa tumeomba kama inaweza ikatoa leseni bado hii inayoelekezwa bodi inayotambua Hotel zinazostahili kutolipa Hotel levy basi watupe muongozo au leseni ambayo inatutambua", amesema mmoja wa wafanyabiashara
Kwa upande wake Afisa Huduma kwa Mlipa Kodi Justine Katiti, amewaomba wafanyabiashara kutoa mapendekezo yao ili kuona sehemu gani inaweza kurekebishwa ili waweze kuyawasilisha ili kupunguza makali ya tozo hiyo.
"Kuna taarifa ambazo wao hawajazipata kwenye bodi ya utalii, kwahiyo tumekubaliana kwamba waainishe yale mapungufu ambayo wameyaona watuletee sisi TRA, tuweze kuyapeleka pale yanapohitajika, ni utaratibu wetu kwamba tukiwa na mabadiliko mbalimbali ya kodi au sheria mbalimbali za kodi tunakutana na wadau wetu kuzungumza nao na na kuwapa maelekezo," amesema Katiti