Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri wa Utalii Zanzibar ateta na Balozi wa Qatar

Waziripicc Data Waziri wa Utalii Zanzibar ateta na Balozi wa Qatar

Thu, 2 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Simai Mohammed Said amemwomba Balozi wa Qatar nchini Tanzania, Hussain Ahmad Al Homaid kusaidia maandalizi ya makala maalumu ya utalii na kurushwa katika kituo cha televisheni cha Al-Jazeera.

Waziri Simai amewasilisha maombi hayo leo Alhamisi Juni 02, 2022 jijini Dar es Salaam wakati wa mazungumzo yake na Balozi Homaid sambamba na kumtunuku cheti maalumu cha kutambua mchango wa shirika la ndege la Qatar Airways katika kuchochea utalii visiwani Zanzibar.

Amesema Tanzania na Qatar zimekuwa na uhusiano mzuri wa kidiplomasia kwa muda mrefu. Hivyo ametumia nafasi hiyo kuiomba Qatar kuwezesha maandalizi ya makala hiyo ya utalii na kurushwa katika kituo cha televisheni cha Al-Jazeera ambacho kinamilikiwa na serikali ya Qatar.

“Tumezungumza na nimemwomba Balozi aweze ku-facilitate (kuwezesha), njia gani tunaweza kufanya documentary (makala) nzuri Zanzibar na Tanzania kwa ujumla ili kuonyesha vivutio katika sekta ya utalii lakini pia sehemu za historian a utamaduni.

“Pia, nimemwomba Balozi atusaidie katika suala zima la heritage management, lakini pia kuwachukua vijana wetu kuwapeleka Doha wakapatiwa mafunzo katika utalii, yakiwa ni ya miezi mitatu au sita,” amesema Waziri Simai.

Waziri huyo ameongeza kuwa mwaka huu kuna mashindano ya Kombe la Dunia ambayo yatafanyika nchini Qatar, hivyo amemwomba Balozi huyo kushirikiana na serikali ya Tanzania ili kuwezesha watalii kuja kutalii Zanzibar na Tanzania wakati wakisubiri mechi wanazotaka kutazama.

Advertisement Kwa upande wake, Balozi Homaid amesema hii ni mara yake ya kwanza kuja kufanya kazi Afrika lakini amejionea uzuri wa bara hili na hifadhi zilizopo tofauti na dhana iliyojengeka huko nje kuhusu Afrika kwamba ni bara lenye njaa, vita na magonjwa.

“Zanzibar ni sehemu nzuri, nimeitembelea mara kadhaa. Ukitembelea Zanzibar utakuta utamaduni wa kiarabu, kwa hiyo huwa tunajisikia tuko nyumbani,” amesema Balozi huyo wakati wa mazungumzo yao.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Utalii ya Zanzibar, Hafsa Mbamba amesema Zanzibar ina uwezo wa kutosha wa kuhudumia watalii kwa sababu kuna zaidi ya hoteli 700 zikiwemo hoteli 40 zenye hadhi ya nyota tano.

“Uwezo wetu ni mkubwa, watalii wengi wanaweza kupata huduma bora wakiwa Zanzibar. Hatuna wasiwasi wa kuelemea, tunajitosheleza,” amesema Mbamba.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live