Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri wa Madini wa Tanzania anguruma kwa dakika tano Paris

63345 Pic+biteko

Wed, 19 Jun 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Paris. Serikali imeahidi kuendelea kutekeleza sera ya uwazi na uwajibikaji katika ulinzi na matumizi ya rasilimali ya Taifa kwa lengo la kuwanufaisha wananchi na Taifa.

Akihutubia mkutano wa nne wa Kimataifa wa tathmini ya mkakati wa Uwazi na Uwajibikaji katika Ulinzi wa Rasilimali za nchi (EITI) jijini Paris, Ufaransa jana Juni 18, 2019, Waziri wa Nishati na Madini, Dotto Biteko ametaja moja ya mafanikio yaliyofikiwa kuwa ni urasilimishaji wa shughuli za wachimbaji wadogo wa madini.

“Mpango huo unaohusisha Serikali, wachimbaji wadogo na wadau wengine wa sekta ya madini, umefanikishwa na uwepo wa sheria na uwazi na uwajibikaji iliyotungwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, mwaka 2015. Mchango wa sekta ya madini kwenye pato na uchumi wa Taifa umeanza kuongezeka,” amesema Biteko.

Katika hotuba yake ya dakika tano kwa wajumbe, Waziri Biteko anayeongoza ujumbe wa Tanzania katika mkutao huo ameahidi kuwa Serikali itaendelea kutekeleza makubaliano ya Kimataifa kuhusu uwazi na uwajibikaji katika sekta na nyanja zote za kiuchumi.

Mwenyekiti wa Kamati ya EITI Tanzania (TEITI), Ludovick Uttoh emetaja moja ya faida ya uwazi na uwajibikaji katika ulinzi na matumizi ya rasilimali za Taifa ni kutoa fursa na haki kwa wananchi kupata taarifa muhimu za miradi inayotekelezwa katika maeneo yao.

Mjumbe wa EITI Tanzania, Blandina Sembu ametaja uzingatiaji wa masuala ya jinsia, hasa umiliki na matumizi ya ardhi kwa wanawake kuwa miongoni mwa faida na mafanikio yanayotokana na utekelezaji wa sera ya uwazi na uwajibikaji katika usimamizi na matumizi ya rasilimali.

Pia Soma

Akifungua mkutano huo, Mwenyekiti wa EITI, Fredrik Reinfeldt amesisitiza umuhimu wa uwazi na wajibikaji katika usimamizi na matumizi ya rasilimali za Taifa kutokana na mafanikio yaliyopatikana tangu mikakati hiyo ilipoanza kutekelezwa.

Mratibu wa Taasisi ya Haki Rasilimali ya Tanzania, Recho Chagonja amesema Mataifa ya Afrika ambao ni wadau wakubwa wa utekelezaji wa mpango huo yanatakiwa kufanyia mabadiliko baadhi ya sera na sheria zake ili kuongeza uwazi na uwajibikaji kwenye rasilimali za Taifa.

Chanzo: mwananchi.co.tz