Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri mpya wa Kilimo alivyotua Mtwara na msimamo wa Serikali

27072 Pic+mtwara TanzaniaWeb

Wed, 14 Nov 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mtwara/Ruvuma. Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga amesema bei ya Sh3,300 watakayolipwa wakulima katika manunuzi ya korosho haitakuwa na makato yoyote, huku akiwataka wanaodai makato hayo kusubiri Serikali itakapotafakari upya.

Waziri Hasunga aliyeapishwa juzi kuchukua nafasi ya Charles Tizeba aliyeenguliwa sambamba na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Charles Mwijage aliyasema hayo jana mara baada ya kufika Mtwara akiwa ameongozana na naibu wake, Innocent Bashungwa na katibu mkuu wa wizara hiyo, Mathew Matigumwe.

Mara baada ya kukagua ghala la Chama cha Ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu), Waziri Hasunga alisema kipaumbele ni kuwalipa wakulima kwanza kabla ya yote.

Hasunga pia aliwataka wafanyabiashara waliotaka kununua korosho kukaa pembeni kwa kuwa walishapewa muda wa kutosha na hawakutumia.

“Korosho yote sasa itanunuliwa na Serikali, lakini kwa kuwa bei imeshuka duniani na hatujui mpaka lini, tumeona angalau kwanza tuanze na mwananchi wa kawaida yaani yule mkulima tumpe hela yake kwanza ili aendelee kulima asije akaathirika. Kwa wiki hii tunataka kuhakikisha wakulima walipwe leo, wiki hii,” alisema Hasunga.

“Mkulima analipwa Sh3,300. Sasa naelewa mkulima anaweza kulipwa, lakini alikopa kwa Juma, kwa Abdallah, sasa haya madeni malizaneni huko, sisi kazi yetu tunayofanya ni kumlipa na wewe kama unajua unamdai umfuate huko. Tusingependa kusikia mara nini, sisi tunataka kwanza apate hela yake,” aliongeza.

Akifafanua zaidi Waziri Hasunga alisema watu wanaowadai makato wakulima wasubiri baadaye.

“Ningependa kutoa ufafanuzi kabla sijaulizwa, tunajua wakulima wanadaiwa makato mbalimbali, hayo itabidi wasubiri baada ya wiki moja tutakaa tuangalie tena,” alisema Hasunga.

Kuhusu hilo, mhasibu mkuu wa Tanecu, Rajab Chambezi alisema katika kilo moja, mkulima anatakiwa akatwe Sh100 ya chama cha ushirika, Sh46 ya halmashauri na Sh45 ya usafirishaji japo inaweza kuongezeka kulingana na umbali.

Alisema kwa upande wa wanunuzi wanatakiwa kukatwa Sh38 za ghala na Sh 52.5 za magunia.

Awali akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Waziri Hasunga alisema anategemea malipo ya wakulima yaanze kulipwa leo.

“Tunataka kuanzia kesho (leo) wakulima wapewe fedha zao, tumeshaandaa fedha zipo,” alisema Waziri Hasunga.

Alifafanua licha ya Benki ya Maendeleo ya Kilimo kutokuwa na matawi mikoani, wakulima watapewa kupitia akaunti za benki wanazohudumiwa au kwa hundi.

“Sisi kama Serikali tunatamani kila mkulima apewe fedha zake, lakini akipewa fedha taslimu kama Sh5 milioni inaweza kuwa hatari kiusalama. Nimeambiwa kila mkulima ana akaunti ya benki,” alisema.

“Tunachotaka wakulima wapate fedha kwanza,” alisisitiza.

Alisema wamelenga kuangalia ubora wa maghala yaliyopo na ukubwa wake ili kuona uwezekano wa kuona  uwezekano wa kuongeza.

“Tunataka kujua hata maghala yanamilikiwa na nani?”

He, ni watu binafsi, bodi au vyama vya ushirika?,” alihoji.

Kuhusu ubanguaji, Hasunga alisema mkakati uliopo ni kuzibangua korosho zote na kuiuza nchini.

Awali, wakitoa takwimu, kaimu mrajisi wa ushirika wa mkoa huo, Salum Issa alisema chama cha ushirika cha Tandahimba na Newala (Tanecu) kina jumla ya tani 35,63465, huku mwakilishi wa chama cha Masasi na Mtwara (Mancu), Potency Rwiza akisema kina jumla ya tani  35,043,055.

Kuhusu malengo yaliyojiwekea, Hasunga alisema ni pamoja na wingi wa korosho na maghala yaliyopo kama yanatosha.

“Hilo ndiyo lengo la ziara yetu, tunataka kuhakiki hizi takwimu tulizoletewa ofisini kwamba tuna tani 103 ayari, ni kweli tunayo kweli? Tumekuja wizara nzima ili tutekeleze maagizo ya Rais. Hapa naona mna tani 72,000,” alisema Waziri Hasunga.

Alisema wanataka kuangalia tani walizonazo zina ubora gani.

“Tunajua korosho ikishavunwa huwa wanaipanga kwa madaraja, sisi tunataka kuhakiki zina ubora gani,” alisema.

Alisema nia wanalenga kuangalia ubora wa maghala ya kuhifadhi korosho hizo ambapo pia alisema wataangalia umiliki wa maghala hayo kama ni watu binafsi au vyama vya ushirika.

“Tunataka kuangalia uwezo wa mghala yetu, yana uwezo wa kuhifashi tan ngapi na je tutahitaji maghala mengine?

Yanamilikiwa na nani? Mangapi yako kwenye vyama vya ushirika? Mangapi yanamilikiwa na Bodi na mangapi sekta binafsi na je tuongeze mangapi?” alihoji.

“Jambo la tatu kama mlivyosikia Mheshimiwa Rais alifanya uamuzi mgumu kwamba korosho zote zilizoko kwenye maghala na ambazo tunazikusanya tutazisimamia wenyewe, tutazinunua,” alisema.

Wanajeshi kuingia Mtwara

Akizungumza operesheni ya jeshi, Hasunga alisema askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wangeingia jana jioni tayari kwa kuweka ulinzi wa maghala yenye korosho, huku Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Gelasius Byakanwa akisema: “Kila ghala litalindwa na askari watatu.”

Byakanwa pia aliwataka wenye maghala hayo kutoingiza korosho nyingine zisizo na ubora ikiwa pamoja na korosho zinazotoka nchi ya Msumbiji.

Wakati Waziri Hasunga akitembelea Wilaya za Mtwara, Tandahimba, Newala na Masasi, Naibu wake alikwenda Liwale Lindi huku Katibu Mkuu akitembelea Mkoa wa Lindi.

Tani 17 zataifishwa, 45 mbaroni

Wakati hayo yakiendelea Lindi na Mtwara, wilayani Tunduru mkoa wa zidi ya tani 17 za korosho zenye thamani ya Sh56.1 milioni zilizokamatwa kisha kutaifishwa.

Akizungumza na Mwananchi jana, Mkuu wa wilaya ya Tunduru, Juma Homera alisema watu hao wamekamatwa nyakati tofauti  kwenye operesheni maalum ambayo inaendelea ya kamata walanguzi ambao wanawalaghai wakulima na kununua korosho kwa mfumo usio rasmi maarufu kangomba ambapo walanguzi uwarubuni wakulima na kununa korosho zao kwa bei ya Sh1000 kwa kilo.

Alisema serikali ipo macho na itahakikisha inawachukulia hatua wafanyabiashara  wote ambao wanajihusisha na biashara hiyo kwani haipo tayari kuona wananchi wakionewa na kuendelea kudidimizwa na walanguzi ambao wanajinufaisha kupitia wakulima hao.

Alisema baadhi ya wafanyabiashara wasio waaminifu wanapeleka fedha nyingi wilayani humo kwa lengo la kununua  korosho  kwa njia ya kangomba wakati wakijua serikali imeshazuia .

“Tumejipanga kuhakikisha mkulima haibiwi korosho zake kikosi kinaendelea kuwafuatilia watu wote na tunafanya kazi mchana na usiku na tunahakikisha tunawakamata wote ambao wanahusika na kuwafikisha mahakamani,” alisema Homera



Chanzo: mwananchi.co.tz