Dodoma. Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa ametaja mikakati atakayoanza nayo baada ya kuteuliwa kuongoza wizara hiyo ikiwa ni pamoja na kufumua mfumo mzima wa utendaji kazi.
Bashungwa alisema hayo jana katika kikao kazi na wakuu wa taasisi 16 zilizo chini ya wizara yake, ikiwa ni wiki moja tangu Rais John Magufuli amteue kuwa katika waziri wa wizara hiyo kuchukua nafasi ya Joseph Kakunda ambaye uteuzi wake ulitenguliwa.
Aliitaja mikakati hiyo kuwa ni Mpango wa maboresho ya mazingira ya biashara (blue print), kufanya upya mapitio ya sera na sheria, kuweka utaratibu wa masoko ya mazao na kutumia fursa zake.
Juni 12, Ikulu jijini Dar es Salaam wakati Rais Magufuli akimwapisha, alitaja sababu za kumuondoa Kakunda kuwa ni kushindwa kutafuta soko la korosho kwa msimu wa mwaka jana.
Serikali iliamua kununua korosho zote za wakulima kwa bei ya Sh3,300 baada ya kushindwa kuelewana na wafanyabiashara waliodaiwa kutaka kununua kwa bei ya chini.
Katika ufafanuzi wake wa jana, Bashungwa alisema sera zinazosimamia kuwapeleka Watanzania katika uchumi wa viwanda ni za mwaka 2003 na alitolea mfano wa Sera ya Masoko ya Mazao ya Kilimo.
Pia Soma
- UCHOKOZI WA EDO: Simu ya rafiki yangu mlevi kuhusu bajeti
- Mahakama yaridhia kunyongwa aliyeua, kuficha maiti kwenye begi
- Kesi yashindwa kuendelea mshtakiwa kalazwa Muhimbili
Alisema katika kikao hicho wamekubaliana kuwa mwaka wa fedha wa 2019/2020 wafanye na kukamilisha mapitio ya sera na sheria wanazotumia kusimamia viwanda na biashara.
Alisema blue print (mpango wa kuboresha mazingira ya biashara) ina sura mbili za shilingi na kwamba sura mojawapo ni kodi kero ambazo wanaendelea kuziondoa.
“Lakini the other side of the coin (upande mwingine wa shilingi) ni change of mindset (mabadiliko ya mtazamo) ndani ya Serikali, lazima tuwe na mtizamo wa customer care (kumjali mteja) kwa wenzetu wafanyabiashara, wenye viwanda, mfanyabiashara mdogo, wa kati,” alisema.
Alisema wasitegemee kuondoa kodi ambazo ni kero kuwa ndiyo utekelezaji wa blue print, bali kubadilisha mtazamo na wao kama wizara inayosimamia biashara na viwanda, ni wawezeshaji si wachanganyaji.
“Sisi wizara tunatakiwa kuhakikisha tunakuwa mfano wa watumishi katika wizara nyingine kwenye hiyo customer care approach,’’ alisema.
Alisema azma ya Serikali ni kuwasaidia wadau kufika katika uchumi wa kati. Jambo jingine alilosema litafanyiwa kazi ni kusimamia na kuimarisha ushirikiano kati ya wizara na sekta ya kilimo.
“Serikali inaendelea kuweka mkakati wa kuongeza uzalishaji, tumeona kuna haja ya kuwa na mkakati wa pamoja ambao ni one marketing plan (mkakati mmoja wa masoko).
Tulikubaliana tutakaa na bodi za mazao pamoja na Tantrade (Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania) pamoja na EPZA (Mamlaka ya Ukanda wa Uwekezaji) kusaidia haya mazao ya kimkakati kwa kuwa na mipango ambayo si ya kushtukizana,” alisema.
Alisema pia watakuwa na mikakati na utaratibu wa masoko wa kila zao kwa kuwa kila zao lina utaratibu wake wa masoko na sio rahisi kuwa na mkakati mmoja kwa mazao yote.
Alisema ni lazima Tanzania ikaangalia fursa zinazopatikana katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na fursa nyingine Afrika, Kusini mwaka Afrika na duniani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Tume ya Ushindani Tanzania (FCC), Profesa Humphrey Moshi alisema kazi kubwa waliyonayo ni kuwezesha wafanyabiashara na kuhakikisha wawekezaji hawabugudhiwi.
“Lakini kutobughudhiwa (wafanyabiashara) ni lazima nao wafuate sheria lakini pia kuwalinda walaji, na kazi hiyo tunaifanya kwa umakini na kwa uzalendo,” alisema.
Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela), Emmanuel Kakwesi aliwataka wananchi wanaotaka kusajili au kuhuisha biashara zao mkoani Dar es Salaam wafanye hivyo hata kama hawana Vitambulisho vya Taifa kwa kuwa wanaweza kupata huduma hiyo katika ofisi hizo.