Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri azungumzia mwenendo bei ya mafuta

Makambapic Data Februari petroli ilipanda kwa 62%

Thu, 7 Apr 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Waziri wa Nishati, January Makamba amezungumzia mwenendo wa bei ya mafuta katika soko la dunia kuanzia Februari 2021 hadi Februari 2022, akisema athari za vita kati ya Ukraine na Russia zimesababisha mahitaji makubwa ya nishati hiyo katika maeneo mbalimbali.

Makamba ameeleza hayo jana Jumatano Aprili 6, 2022 wakati akitoa taarifa kwa umma kuhusu mwenendo wa upatikanaji wa mafuta baada ya Serikali kutangaza bei mpya za nishati hiyo, zilizoanza kutumika jana.

Katika maelezo yake, Makamba amesema mwenendo wa bei ya mafuta katika soko la dunia kuanzia Februari 2021 Petroli yalikuwa dola 561.74 kwa tani, wakati dizeli dola 503.73 kwa tani na mafuta ya taa  dola 504.21.

"Kufikia Februari 2022 bei za mafuta katika soko la dunia zilikuwa; Petroli dola 911.94 kwa tani sawa na ongezeko la asilimia 62. Dizeli dola 826.14 kwa tani sawa na ongezeko la asilimia 64 ikilinganishwa na bei za Februari 2021 huku mafuta ya taa yakiwa dola 826.35 kwa tani sawa na ongezeko la asilimia 64.

"Ongezeko la bei la mafuta katika soko la dunia linatokana na sababu kuu mbili ya kwanza nchi nyingi duniani kufungua shughuli zake za kiuchumi na kijamii baada ya kupatikana kwa chanjo ya Uviko-19. Kufunguka huku kumefanya ongezeko kubwa la mahitaji ya mafuta wakati uzalishaji wake ni pungufu kwa mataifa yanayozalisha," amesema Makamba.

Amesema jambo jingine ni mgogoro wa kivita kati ya Russia na Ukraine uliopunguza uwepo wa mafuta katika soko la dunia hasa baada ya Nato kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Russia ambayo ni miongoni mwa mataifa 10 yanayozalisha nishati hiyo.

Advertisement “Upungufu huu umesababisha bei za mafuta katika soko la dunia kuongezeka kwa kiwango kikubwa kuanzia Februari 2022. Niwatoe hofu hakutakuwa na uhaba wa mafuta na hakuna haja ya kuwa na taharuki wala kupaniki.

" Mafuta yaliyoko kwenye maghala na vituoni yanatosheleza mahitaji na yataendelea kuuzwa kwa utaratibu wa kawaida hakuna haja ya kuzua taharuki. Mfumo wetu wa uagizaji ni salama na thabiti," amesema Makamba.

Mbali na hilo, Makamba amesema maghala ya mafuta hapa nchini yana mafuta ya kutosha na kila siku nishati hiyo inapokelewa. Amesema kuna meli ambazo ziko njiani kuendelea kuleta mafuta.

“Kufikia  Aprili Mosi mwaka huu mafuta yaliyokuwa kwenye maghala ni petroli  lita 118,594,024 yanatosheleza siku 27, dizeli  lita 116,486,705 yanatosheleza siku 19, mafuta ya taa  lita 6,823,710 yanatosheleza siku 108 na mafuta ya ndege lita 12,841,822 yanatosheleza siku 35,” amesema.

Bei ya petroli yagonga Sh2,861

Chanzo: www.tanzaniaweb.live