Naibu Waziri wa Nishati Judith Kapinga amewasihi Viongozi wa vijiji, Kata na Vitongoji kuwahamasisha Wananchi kujiunganishia huduma ya umeme kwenye nyumba zao ili kutekeleza azma ya Serikali ya kuhakikisha inafikisha nishati ya umeme kwa Wananchi wote
Kapinga amesema hayo wakati akiwasha umeme kwa mara ya kwanza katika kijiji cha Ilambo, kata ya Ibumo, wilayani Kilolo, mkoani Iringa alipofanya ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa Miradi ya usambazaji umeme vijijini leo, Ijumaa Desemba 15.2023
Awali Naibu Waziri Kapinga amesema Jimbo la Kilolo lina jumla ya vijiji 94 ambapo vijiji 93 sawa na asilimia 99 vimepatiwa huduma ya umeme kupitia Miradi ya awali kama vile REA I, REA II na REA III (Mzunguko wa Kwanza) na REA III (Mzunguko wa Pili)
"Jimbo la Kilolo lina jumla ya vitongoji 493 ambapo vitongoji 292 sawa na asilimia 59.22% vimepatiwa umeme, Wakala wa Nishati vijijini umeendelea kutekeleza miradi mbalimbali katika Jimbo la Kilolo ukiwa na lengo la kuwapatia huduma za nishati kwa Wananchi ili kuboresha huduma za jamii na kiuchumi maeneo ya vijijini, vitongojini na kazi ya kusambaza umeme ni endelevu” -N/Waziri Kapinga
Amesema, Serikali imekuwa ikitoa fedha ili kuhakikisha inatekeleza Miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ile ya kusambaza umeme vijijini ili kuwafikia Wananchi wote
"Viongozi wa kata, vijiji na vitongoji ninyi mpo na Wananchi muda wote pia ni daraja kati ya Wananchi na Serikali kuu, hivyo ni vyema kuwahamasisha Wananchi hao kuweka umeme kwenye nyumba zao ambao wamefikiwa na huduma hiyo na wengine kuendelea kuandaa nyumba kwa kusuka nyaya (Wiring) ili kujiweka tayari kwa kuunganishwa na umeme pindi itakapofika katika maeneo yao, tunajua maendeleo ni hatu hivyo kila mmoja atafikiwa na huduma ya umeme, muhimu ni kujiweka tayari muda wote” -N/Waziri Kapinga
Ameongeza kuwa Serikali inapenda kuona Wananchi wake wanapiga hatua za maendeleo kupitia miradi wanayowapelekea hivyo ni busara na vyema kuona miradi inayoitekeleza na kuwafikia wananchi inatumika kwa wananchi
Amewaelekeza Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) pamoja na Wakala wa Nishati Vijiini (REA) kuhakikisha wanaweka utaratibu mzuri wa kuwasaidia Wananchi wanajiunganisha (Wiring) na huduma ya umeme kwa bei nafuu katika nyumba zao ili waifurahie na waone thamani ya Miradi hiyo ambayo inaanzishwa na kuendelezwa na Serikali kwa fedha nyingi
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kilolo Peles Magili amewasisitiza Wananchi kuendelea kutunza na kuilinda miundombinu ya umeme ili itumike kwa muda mrefu
Aidha, amewataka Wananchi kutoa taarifa kwa Mamlaka husika pindi wanapoona mtu yeyote anahujumu au kupanga njama ya kuiba au kuharibu miundombinu ya umeme kwa kuwa Serikali inatumia fedha nyingi kugharamia miundombinu hiyo