Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri ashangaa kupotea kwa sukari

5072 Sugar Kiwanda Waziri ashangaa kupotea kwa sukari

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

WAKATI sukari ikiendelea kuwa bidhaa adimu katika baadhi ya maeneo mbalimbali nchini, serikali imesema haifahamu inapofichwa kwa sababu ipo ya kutosha.

Imesema kwa sababu ya sintofahamu hiyo, wameandaa mpango mkakati wa kuanza kusaka inapofichwa sukari hiyo kuanzia Jumatatu ya wiki ijayo.

Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga, aliyaeleza hayo jana, wakati akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu na kusema kuwa, kinachofanyika ni uhuni kwa sababu bidhaa hiyo ipo kwa wingi nchini.

“Kinachofanyika ni uhuni, kwa sababu sukari ipo ya kutosha, hatuna uhaba wa sukari nchini,” alisema Hasunga.

Alieleza kuwa, kwenye maduka ya jumla hakuna uhaba wa sukari na inauzwa kwa bei elekezi, hali inayoifanya serikali kushindwa kufahamu sababu ya bidhaa hiyo kutowafikia wananchi, lakini kutokuuzwa kwa bei elekezi.

“Hatujui kwa nini sukari iuzwe bei ya juu, wakati ipo ya kutosha, tutapita duka kwa duka kwa ajili ya kufanya ukaguzi wa kubaini wale wote wanaoleta fujo kwenye bidhaa hii,” alisema Hasunga.

Alisema kwa kuanza wataanza na mkoa wa Dar es Salaam, ambako kuna bandari inayoshusha bidhaa hiyo hivyo hakukuwa na sababu yoyote ya kuwa adimu.

Asunga alisisitiza kuwa, watapita katika maduka na maeneo ambako wanadhani kuwa bidhaa hiyo imefichwa na watafika katika mikoa yote nchini.

HALI ILIVYO DAR

Nipashe jana lilipita katika baadhi ya maduka katika jijini la Dar es Salaam zikiwamo ‘Super market’ na kukuta bidhaa hiyo ikiuzwa kwa mashati na wengine wakiuza kwa bei ya kati ya Sh. 3,000 na 4,000.

Katika duka kubwa la Mlimani City jana kilo moja ya sukari ilikuwa ikiuzwa kwa bei elekezi ya Sh. 2,600, lakini kwa masharti ya kila mteja kununua kilo mbili peke yake.

“Nimeenda kununua sukari pale Mlimani City kwa masharti ya kutochukua zaidi ya kilo mbili na wakati natoka ndani pale ikawa ishamalizika kwa hiyo wateja waliongia nyuma yangu walikosa,” alisema mmoja wa wanunuzi wa sukari.

Katika maeneo ya Mwanayamala, sukari inapatikana katika baadhi ya maduka na kwa bei ya kuanzia Sh. 3,500 hadi 4,000 kulingana na matakwa ya muuzaji.

“Unakuta duka hili linauza Sh. 3,600, lingine 3,700 na mengine yanauza 4,000 lakini siyo maduka yote ni baadhi tu ambayo yanauza,” alisema Jumanne Khamis mkazi wa Mwananyamala.

Katika maeneo ya Tabata Segerea, sukari inauzwa katika baadhi ya maduka kwa bei ya Sh. 3,500 na maduka mengine wanauza ikiwa imeshapimwa na kufungwa kwenye vifungashio.

Katika maeneo ya Kimara sukari inauzwa Sh. 3,500 katika baadhi ya maduka, wakati maduka mengine yakiwa hayana bidhaa hiyo.

Nipashe lilipita katika baadhi ya maduka ya jumla na kukuta sukari ikiuzwa kati ya Sh.125,000 na 128,000 kwa kilo 50 kutoka Sh. 140,000 hadi 150,000 kwa siku za nyuma.

Itakumbukwa kuwa, Mei 14, mwaka huu, Waziri wa Viwada na Biashara, Innocent Bashungwa, alipokea shehena ya tani 600 ya sukari katika bandari ya Mwanza ikitokea nchini Uganda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live