Dodoma. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ina upungufu wa watumishi 2,249 ili kufikia idadi ya watumishi 7000 wanaohitajika nchi nzima.
Hayo yameelezwa bungeni leo Ijumaa Septemba 13, 2019 na naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Ashatu Kijaji na kubainisha kuwa ni upungufu mdogo.
Dk Kijaji alikuwa akijibu swali la msingi la mbunge wa Viti Maalum (Chadema), Tunza Malapo aliyehoji ni watumishi wangapi wanahitajika TRA ili mamlaka hiyo iweze kufanya kazi zake kwa ufanisi.
Dk Kijaji amesema kwa sasa TRA ina waajiriwa 4,751 ambao wanaendelea na kazi na wakati wowote wataajiri wafanyakazi 150 na wataendelea kuajiri kadri uwezo utakavyoruhusu.
Dk Kijali amesema upungufu uliopo ni wa asilimia 28 na aliahidi kumpatia mbunge mchanganuo wa mahitaji yote kwa waliopo kazini na wanaohitajika.