Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri akutana wadau wa usafirishaji

Waziri Pic Waziri akutana wadau wa usafirishaji

Sun, 19 Dec 2021 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Wiki moja baada ya Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Rahma Kassim Ali kutembelea bandari ya Malindi kukagua hali ya usafirishaji wa abiria na kubaini kasoro kadhaa, amekutana na wamiliki wa vyombo vya usafirishaji kupata mwarobaini wa changamoto zilizobainika.

Miongoni mwa changamoto hizo ni wingi wa watoto chini ya miaka 12 hususani meli zinazofanya safari zake kati ya Unguja na Pemba, abiria kukaa chini badala ya viti na ongezeko la abiria wanaosafiri katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka.

Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika ofisi za Mamlaka ya Usafiri Baharini (ZMA) leo Jumapili Desemba19, 2021, Waziri Rahma amesema lengo ni kuleta tija katika usafirishaji wa abiria na mizigo yao.

“Siku chache tulifanya ziara tukatembelea meli tuliona namna hali ilivyo, watoto ni wengi zaidi ikilinganishwa na idadi ya biria, lakini abiria ni wengi kwa kipindi hiki wapo wanaobaki kwa kukosa usafiri kwahiyo tunataka kuona njia bora ya kushughulikia masula haya,”amesema Waziri Rahma

Amewaomba wamiliki hao kuangalia njia nzuri ya kuongeza vyombo vya usafiri ili kuwaepushia adha abiria wanaosafiri kutokana na wingi wao huku kukiwa na baadhi yao wanaouziwa tiketi na vishoka jambo linaloongeza wingi wao ndani ya meli.  

Naye katibu Mkuu wa wizara hiyo, Amour Hamil Bakari amesema suala la abiria kukaa chini badala ya kukaa kwenye viti, sio tu halipo vizuri kiusalama lakini halileti haiba ndani ya meli.

“Ukaaji chini kwenye meli kiusalama, kimazingira sio sawa kabisa, kwanza kuna maradhi mengi hasa zaidi kwa sasa kuna maradhi haya ya Covid-19 maana watu wanasongamana hata pakupitisha mguu hakuna,” amesema Bakari

Mkurugenzi wa kampuni ya Ikraam Sealine, Abdulghafour Ismail amesema wao tayari wameshazingatia suala la kupunguza adha ya wasafiri kwa kuongeza ruti ya safari kati ya Pemba na Unguja ambapo wanaenda mara tatu, “siku moja kwenda siku moja kurudi.”

Meneja wa Operesheni wa kampuni ya Zan Fest Feries, Rashid Aley mesema ni vyema mamlaka ikaangalia njia bora ya kuruhusu baadhi ya meli kuchukua idadi kubwa ya abiria kupunguza adha hiyo.

Amesema zipo baadhi ya meli zina uwezo mkubwa lakini zimewekwa kiwango kidogo cha kubeba abiria “mfano sahivi meli inachukua abiria 500 lakini ina uwezo wa kubeba abiria zaidi ya 900.”

Ombi kama hilo lilitolewa na mwakilishi wa meli ya Flying Horse, Nasrullah Morawej alisema waruhusiwe kubeba abiria 425 badala ya 400.

Naye Meneja Mkuu wa kampuni ya Aje Marine Ltd, Seif Hemed ameomba utaratibu wa kuruhusu meli zisafirishe abiria wakati wa usiku urejee kama ilivyokuwa zamani, hata hivyo hoja hiyo imepingwa kwa madai safari za usiku sio salama ndani ya bahari.

Chanzo: www.mwananchi.co.tz