Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri aisema Fastjet kiaina, Masha afunguka

Thu, 20 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe amesema mashirika ya ndege yaliyoshindwa kazi hayawezi kurejea tena kwa kuwa Serikali imejipanga.

Kamwelwe alitoa kauli hiyo jana katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la upanuzi wa barabara ya Morogoro jijini Dar es Salaam katika eneo la Kimara Stop Over uliofanywa na Rais John Magufuli.

“Mheshimiwa Rais, ukishapokea ndege mpya, tumeshajipanga ndege moja itaanza kuruka tarehe 26 mwezi huu siku ya Boxing Day. Hakutakuwa na upungufu wowote,” alisema Kamwelwe.

“Na sisi tutahakikisha anayeshindwa atashindwa moja kwa moja na mpaka alegee na harudi kwa sababu tumejipanga.”

Alitoa kauli hiyo saa chache baada ya mwenyekiti mtendaji wa Shirika la Ndege la Fastjet Tanzania, Lawrence Masha kueleza kuwa anatarajia kuingiza ndege mbili zitakazorejesha huduma zake.

Masha alitoa kauli hiyo alipokuwa akihojiwa na kituo cha runinga cha Clouds.

Alisema Jumamosi wiki hii ataingiza ndege nyingine aina ya Boeing 737 kwa ajili ya kuliinua shirika hilo ambalo sasa shughuli zake zimesitishwa.

“Ndege zote zitakuwa na usajili wa Tanzania na kutokana na mahitaji tunaweza kuongeza ndege nyingine moja au mbili aina ya Bombardier.”

Masha alisema ndege ya Fastjet aina ya Boeing 737 ambayo imezuiwa kuruka na Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) kutokana na hitilafu za kifundi sasa iko imara na inaweza kutoa huduma.

“Tunatarajia kurejesha safari za Nairobi na Afrika Kusini kuanzia Februari mwakani. Pia, tutaanzisha safari za Songea, Dodoma, Bukoba na Arusha mjini endapo TCAA wataturuhusu kwa kuwa tutakuwa na ndege ndogo ambazo zina uwezo wa kutua katika viwanja hivyo,” alisema Masha.

Alisema baadhi ya wafanyakazi wamelipwa mishahara yao ya Desemba juzi na wengine wangelipwa jana huku malipo ya watoa huduma kwa shirika hilo yakiandaliwa na kwamba Fastjet Plc imekubali kuyalipa baadhi ya madeni.



Chanzo: mwananchi.co.tz