Biashara

Habari

Burudani

Michezo

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Waziri afafanua sakata la samaki kupimwa kwa rula

Thu, 12 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Ashauri wananchi watumie fursa ya ufugaji bora wa samaki

Dar es Salaam. Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega amewataka wananchi wasikatishwe tamaa na suala la samaki kupimwa kwa rula badala yake watumie fursa ya ufugaji samaki bila hofu.

Alisema hayo alipokuwa kwenye banda la kilimo na uvuvi.

“Suala la kupima samaki kwa rula linahitaji elimu kidogo. Halihusishi kila samaki, linawahusu wale wanaovuliwa kwenye Ziwa Victoria pekee,” alisema Ulega.

Alifafanua kuwa hata kwa wale watakaofuga samaki wanaopatikana katika ziwa hilo wasiwe na hofu kwa sababu kuna taratibu za ufugaji katika maeneo waliyopo.

“Kuna watu wanaohusika na mifugo kwenye maeneo tunayoishi, hivyo unapofuga unapaswa kuwasiliana nao ili wakutambue na kukuthibitishia kuwa unafuga katika eneo hilo, ili jambo lolote likitokea kuhusu samaki wako, uwe na mtetezi kama siyo kibali. Fugeni samaki hii ni fursa na inatoa ajira, inaongeza kipato na inaboresha afya za walaji,” alisema Ulega na kushauri namna bora ya kutunza majani kwa wafugaji wa ng’ombe.

Aliwataka wananchi watembelee banda hilo ili waelekezwe namna bora ya kutunza majani kwa ajili ya mifugo yao.

Alisema kwamba Februari, Machi na Aprili mvua huwa zinanyesha na majani yanakuwa mengi, baada ya hapo linakuja jua na kunakuwa na uhaba wa bidhaa hiyo muhimu kwa mifugo.

“Sasa katika banda la mifugo na uvuvi wapo wataalamu wa kuelekeza namna ya kuyatunza majani wakati wa msimu wa Masika yatakayotumika wakati wa kuangalia,” alisema Ulega.

Chanzo: mwananchi.co.tz